Na Carlos Claudio, Dodoma📍.
NAIBU Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Reuben Kwagilwa, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga fedha maalumu kwa ajili ya mafunzo ya watumishi wake ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza Desemba 5 katika mahafali ya 17 ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo (LGTI) jijini Dodoma, Kwagilwa alisema mafunzo ya muda mfupi yamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo watumishi wanaochaguliwa na kuteuliwa, hivyo ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha rasilimali hizo zinatengwa kila mwaka.
“Kupitia mafunzo haya watumishi watatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa tija. Kwa niaba ya Waziri Mkuu, naelekeza sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinakitumia chuo hiki kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam utakaosaidia kutatua changamoto katika maeneo yao,” alisema.
Aidha, aliutaka uongozi wa chuo kuhakikisha unaendelea kuimarisha mazingira ya kazi kwa watumishi wake wanaoongezeka pamoja na kuongeza motisha kwa wanaofanya vizuri ili kuendeleza ari ya utumishi wenye weledi.
“Hakuna haki bila wajibu. Naomba watumishi wa chuo muendelee kuwajibika na kuzingatia kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009,” alisisitiza Kwagilwa.
“Vyeti ni karatasi tu, lakini maarifa mliyopata ndiyo yanayopaswa kutafsiriwa kwenye kazi zenu. Tunawatakia heri, mkafanye kazi kwa weledi na kuacha alama,” alisema Shekimweri.
Aidha, aliwapongeza wanafunzi wanaoendelea na masomo kwa kudumisha utulivu chuoni hapo na kueleza kuwa Chuo cha Serikali za Mitaa kimekuwa msaada mkubwa kwa wilaya hiyo katika kutoa semina elekezi kwa viongozi, ikiwemo madiwani wa Jiji la Dodoma.
Alisema sambamba na kuongeza programu mpya za masomo, chuo kimekuwa mstari wa mbele kutatua changamoto za jamii ikiwemo kusogeza huduma ya maji safi kwa wananchi wa maeneo yanayokizunguka chuo.
Aidha, tangu mwaka 2015 chuo kimekuwa na utaratibu wa kudahili na kufadhili wanafunzi kutoka familia zisizo na uwezo katika mtaa wa Hombolo Bwawani, ambapo kwa sasa idadi imeongezeka kutoka wawili hadi wanne kwa mwaka.
Dk. Yusuphu alisema chuo pia kinaendelea kutoa huduma ya afya ya mama na mtoto kwa wakazi wa eneo hilo, pamoja na kuendelea kushiriki michezo mbalimbali ya kitaifa na kirafiki kwa ajili ya kujenga afya na mahusiano mema na taasisi nyingine.
“Zaidi ya wahitimu 5,000 wamefaidika na mafunzo ya Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani za Maendeleo ya Jamii, Utawala na Rasilimali Watu, pamoja na Usimamizi wa Fedha na Manunuzi kwa Serikali za Mitaa,” aliongeza.












