JAWADU: VIJANA MLINDE HESHIMA YA RAIS NA AMANI YA TAIFA – DODOMA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Jawadu Mohamed, ametoa wito kwa vijana wote wa Tanzania, bila kujali itikadi zao za kisiasa, kuhakikisha wanalinda heshima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoshiriki katika mipango yoyote yenye kuvuruga taswira ya taifa.


Akizungumza leo Desemba 11, 2025 jijini Dodoma na waandishi wa habari pamoja na wananchi, Jawadu amesema kumchafua Rais wa nchi ni sawa na kulichafua taifa lote, kwani Rais ni nembo na utambulisho wa nchi mbele ya dunia.


“Katika hali ya kawaida na kwa ushahidi wa kiakili, Rais wa nchi ni nembo ya taifa. Hakuna namna unaweza kumhujumu Rais bila kulihujumu taifa. Ukimchafua Rais, basi watanzania wote tumepata doa,”amesema Jawadu.


Jawadu alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujiepusha na propaganda, uchochezi na tafrani zinazolenga kuvuruga amani, akiwapongeza vijana wa Dodoma kwa jinsi walivyokataa vurugu zilizodaiwa kuandaliwa Oktoba 29 na Desemba 9.


“Ardhi yenye vurugu haistawishi chochote. Hakuna anayepata faida katika machafuko. Tunapaswa kuwekeza kwenye utulivu, kuheshimu viongozi na kutoa ushauri kwa njia stahiki,” aliongeza.


Katika kuelezea umuhimu wa umoja wa kitaifa, Jawadu alisema hakuna mtu anayeweza kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini, siasa, kabila au kipato, kwani Watanzania wana uwezo wa kutatua changamoto zao wakiwa katika nchi yenye amani na kwa kushirikiana na viongozi wao.


Akimzungumzia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche, Jawadu alisema kauli zozote zinazodai kuwa Rais si halali hazina mashiko, kwa kuwa Dkt. Samia alichaguliwa na zaidi ya Watanzania milioni 32, huku dunia yote ikiwa inamtambua.


“Vyama vyovyote vinavyoenda kinyume na uhalisia vitaendelea kupoteza mvuto. Dunia ya sasa inataka vyama vinavyoongozwa kwa hoja, ukweli na uhalisia,” amesema.


Baadhi ya wakazi wa Dodoma waliunga mkono wito wa kudumisha amani na kumheshimu Rais.


Stephanon Silayo, mkazi wa Dodoma, alisema Watanzania wanapaswa kuungana na serikali katika kipindi hiki cha maridhiano, akibainisha kuwa vijana wamepewa nafasi za kutoa maoni yao ndani ya serikali, ikiwa ni hatua ya kujenga taifa la ushirikiano.


“Tuiunge mkono serikali, tusiingie kwenye vurugu. Vinapotokea vurugu wanaoumia ni sisi watu wa chini. Viongozi wanaotuchochea wao wanabaki salama,” amesema Silayo.


Collinel Mtui, mkazi mwingine wa Dodoma, aliwataka vijana kuacha kufuata mkumbo wa kauli zisizo na tija na badala yake kujikita katika maendeleo.


“Uchaguzi umepita, Rais ni Dkt. Samia na anatambulika kikatiba. Vijana tufanye kazi na kujenga uchumi wa nchi,” amesema Mtui.


Jawadu aliwataka vijana kuongeza uzalendo na kuendelea kulinda amani, akiongeza kuwa amani ndiyo msingi wa mafanikio ya taifa na maendeleo ya vijana wenyewe.







🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post