MAPINDUZI YA TEHAMA KUIONGOZA TANZANIA KUFIKIA DIRA YA MAENDELEO 2050

 


Na Carlos Claudio, Dodoma📍.


Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesisitiza dhamira yake ya kuifikisha Tanzania katika hatua mpya ya maendeleo ifikapo mwaka 2050, kupitia mapinduzi ya teknolojia na kuondoa urasimu kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi, hasa katika ngazi za Serikali za Mitaa.


Akizungumza leo Desemba 4, 2025 katika Kongamano la 17 la Mapinduzi ya TEHAMA lililofanyika katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu — TAMISEMI, Erick Kitali, amesema serikali inatekeleza maboresho makubwa yatakayohakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu. 



Kitali amesema mapinduzi hayo yanagusa sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji wa mapato, utoaji wa vibali na leseni kidijitali, uuzaji wa viwanja, pamoja na mifumo ya elimu inayowawezesha wadau kufahamu idadi ya wanafunzi waliopo mashuleni na waliopo nje ya mfumo kwa ajili ya ufuatiliaji.


“Yote haya yakijumuishwa na yale wanayojifunza darasani pamoja na mifumo tunayoitumia, tuna uhakika kwamba tunakwenda kuipata Tanzania tunayoitarajia ifikapo mwaka 2050,” amesema Kitali.


Aidha, amebainisha kuwa maelekezo ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hadi kufikia mwaka 2030 yanataka ofisi hiyo ihakikishe Watanzania wanapata “Tabasamu” kwa kupunguza urasimu, kuchelewesha huduma na kuongeza uwazi, huku watumishi waliofundishwa vizuri wakitumia teknolojia ya kisasa katika kuwahudumia wananchi.



Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo cha Serikali za Mitaa  Hombolo, anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Profesa Magreth Bushesha, amesema mifumo ya TEHAMA imeleta maboresho makubwa katika utoaji huduma, lakini bado kuna uhaba wa wataalam. Amewahimiza wadau kuongeza juhudi katika kuandaa wataalam wa kutosha ili kwenda sambamba na kasi ya teknolojia.


“Sisi kama chuo tumeanzisha programu mpya za ICT ili kuchangia maendeleo na kuongeza ubora katika utoaji wa huduma kwenye mamlaka za serikali za mitaa,” amesema Profesa Bushesha.



Naye Profesa Frank Theobard kutoka Taasisi ya Stadi za Maendeleo, Chuo Kikuu cha Mzumbe, ameitaka serikali kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya TEHAMA, akibainisha kuwa dira mpya ya maendeleo ya miaka 25 (2025–2050) inalenga kuboresha ustawi wa wananchi kupitia huduma bora za kijamii.


Kwa mujibu wa Profesa Theobard, “Tanzania imepiga hatua kubwa katika TEHAMA, na serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kutumia teknolojia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii.”



Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachuo waliobainika kufanya vizuri katika masomo yao, akiwemo Stera Muyengi, Musa Mkumbo, Angelo James na John Dominica wamesema mafanikio yao yametokana na bidii, kusikiliza walimu, ushirikiano kutoka kwa wazazi na wanafunzi wenzao pamoja na kumtegemea Mungu.


Kongamano hilo la 17 lililoandaliwa na Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo limebeba kaulimbiu isemayo: “Mabadiliko ya kidijitali kwa utoaji wa huduma za serikali za mitaa nchini Tanzania: kichocheo cha kufanikisha Dira ya 2050.”














🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post