Na Jasmine Shamwepu Dodoma.📍
Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Warioba Butiku, amesema kuwa licha ya vijana kuwa na hoja nyingi zenye msingi katika kujenga taifa, si sahihi kuziwasilisha kupitia maandamano au vitendo vya vurugu vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi.
Akizungumza katika kikao cha viongozi wa dini na wazee kuhusu ujenzi wa umoja, haki na amani kilichofanyika jijini Dodoma, Mzee Butiku alisema kuwa Tanzania imeendelea kudumisha amani kwa kuzingatia misingi ya usawa, heshima, haki na kutokubaguana, hivyo akawahimiza vijana kutumia njia rasmi na za kikatiba kuwasilisha changamoto zinazoikabili jamii.
Aliongeza kuwa wazee hawako kinyume na hoja za vijana, bali wanazitambua na kuziheshimu, ndiyo maana wamekuwa wakihimiza mazungumzo ya wazi na yenye maridhiano kati ya pande husika.
Butiku aliwataka vijana, wazee na viongozi kuendelea kushirikiana na kuwasiliana kwa njia ya maridhiano na hekima, akisisitiza kuwa bado wazee wana nafasi kubwa ya kusaidia taifa kutatua changamoto hata pale panapokuwepo tofauti za mawazo.
Alisisitiza kuwa kudumisha amani na umoja wa kitaifa ni jukumu la kila Mtanzania, na kwamba njia ya mazungumzo na utaratibu wa kikatiba ndiyo nguzo muhimu ya kujenga taifa imara na lenye mshikamano.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.





