Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza hospitali zote nchini kuhakikisha wajawazito wanapewa huduma za haraka mara wanapofika hospitalini ili kuokoa maisha ya mama na mtoto. Agizo hilo amelitoa leo, Novemba 15, 2025, wakati wa ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Amesema haiwezekani mjamzito kufika hospitalini na kukaa muda mrefu bila kuhudumiwa, huku akisisitiza kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha huduma za afya kupitia uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Katika maelekezo mengine, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Afya, Bohari ya Dawa (MSD) na hospitali zote za umma kuweka kipaumbele katika upatikanaji wa dawa kulingana na mahitaji ya maeneo yao.
“Haipendezi mwananchi kufika hospitali na kupatiwa vipimo kisha kuambiwa aende kununua dawa nje. Kama duka binafsi linaweza kupata dawa, inakuwaje hospitali za serikali hakuna? Naagiza hospitali zote ziwe na dawa,” amesema.
Dkt. Mwigulu pia ameelekeza hospitali zote kuwa na vifaa vya usafi binafsi vya dharura, ikiwemo ndoo na mabeseni katika wodi za wazazi ili kuwasaidia akinamama ambao hawana vifaa hivyo. Ameeleza kuwa ujauzito si dharura inayotokea bila utayarifu; hivyo vifaa hivyo vinapaswa kupatikana muda wote.
Akizungumza na wananchi nje ya hospitali baada ya kutembelea wodi mbalimbali, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na namna wananchi wanavyoendelea kuhudumiwa, na kumpongeza Rais Samia kwa kuimarisha mifumo ya afya, vifaa tiba na upatikanaji wa dawa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amezielekeza hospitali nchini kutumia mifumo rasmi ya malipo ili kuhakikisha Serikali inapata mapato sahihi kwa ajili ya kuendelea kuboresha huduma. Amesema bado kuna hospitali zinazotoza malipo nje ya mifumo ya kidijitali, jambo ambalo halikubaliki.
Wananchi na wagonjwa waliokutana na Waziri Mkuu hospitalini hapo wamemshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tunapatiwa huduma nzuri kama tupo hospitali za binafsi,” amesema Dinna Enock, mkazi wa Makulu jijini Dodoma, aliyelazwa katika wodi ya wazazi.
Waziri Mkuu ameendelea kusisitiza usimamizi mahiri na uwajibikaji katika sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.


