Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Foundation Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amepongeza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa bungeni, akisema imeleta mwanga mpya kwa taifa lililokuwa limetoka kwenye kipindi kigumu cha uchaguzi.
Ametoa pole kwa Watanzania wote kutokana na changamoto, taharuki na maumivu yaliyowakumba, akisisitiza kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia, nchi itapita salama na kurejea kwenye misingi imara ya mshikamano wa kitaifa.
Salali amesema hotuba ya Rais imekuwa ni majibu ya matarajio ya mamilioni ya Watanzania, hususan katika maeneo ya kuponya majeraha, kurejesha imani ya wananchi, na kufungua ukurasa mpya wa maridhiano ya kitaifa.
Kwa mujibu wake, hotuba hiyo ilisubiriwa kwa hamu kubwa na imeondoa maswali mengi yaliyokuwa yakizungumzwa na wananchi kwa muda mrefu.
“Rais amefungua mlango wa mazungumzo. Hii ina maana kubwa — Tanzania ina kiongozi msikivu, anayejali watu wake na anayetaka kuona nchi inaendelea mbele kwa umoja,” amesema.
Amegusia athari zinazowakumba watu wenye ulemavu wakati wa uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa kundi hilo huwa kwenye mazingira hatarishi zaidi.
Amesema asiyeona hawezi kukimbia hatari, kiziwi hawezi kusikia tahadhari, na watu wengine wenye uhitaji maalum hukosa msaada wa haraka wanapokumbana na vurugu. Hivyo, amani na utulivu ni nguzo muhimu kwa maisha yao.
Salali amepongeza hatua ya Rais Samia ya kutoa msamaha na kuwaachia huru vijana waliokuwa wakishikiliwa na vyombo vya dola, akisema kitendo hicho kimetafsiriwa kama “tiba ya majeraha” kwa taifa na kwa makundi maalum kama watu wenye ulemavu, ambao huathirika moja kwa moja pale amani inapodorora.
Ameeleza kuwa kile alichokiita "kiwanja cha maridhiano" ni nafasi ya Watanzania kujiponya, kurejesha imani na kuimarisha nguvu ya pamoja kama taifa linalotanguliza umoja.
Katika wito wake kwa vijana, Salali amesema wao ndiyo walinzi wakuu wa taifa, hivyo wanapaswa kujilinda kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani au kupandikiza mgawanyiko.
“Tutofautiane kwa mitazamo, hiyo ndiyo demokrasia, lakini tusifike hatua ya kuumiza taifa,” amesisitiza.
Amehimiza kuwa kipindi hiki si cha lawama wala kunyoosheana vidole, bali ni muda wa kurejesha utamaduni wa amani, upendo na umoja — misingi ambayo imeizaa na kuiweka Tanzania katika ramani ya utulivu kwa vizazi vingi.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.
