Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Profesa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na mtaalamu wa elimu maalum na jumuishi, Prof. Cosmas Mnyanyi, amesema mradi wa Ninakusikia umeonyesha matokeo makubwa katika kubaini na kutatua changamoto za usikivu kwa watoto nchini.
Lengo kuu la mradi huo ni kuhakikisha watoto wenye matatizo ya kusikia wanatambuliwa mapema na kusaidiwa ili wafanye vizuri katika masomo na maisha kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa matokeo ya awamu ya pili ya utafiti huo, Prof. Mnyanyi alisema mradi ulianza mwaka 2017 kwa ushirikiano wa OUT, Chuo cha Ualimu Patandi, KCMC na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika awamu ya kwanza, jumla ya watoto 616 walifikiwa, huku utafiti wa awali (pilot) ukifanyika kwa wanafunzi 403 kutoka shule tatu, mbili zenye wanafunzi wenye ulemavu na moja ambayo jamii yake ilikuwa ikiamini hakuna mtoto mwenye changamoto.
“Katika ile shule ambayo waliamini hakuna changamoto, tulikuta asilimia 17% ya watoto wana tatizo la kusikia,” alisema Prof. Mnyanyi. “Tuligundua kwamba mengi ya matatizo haya yanaweza kutatuliwa mapema na mtoto akapona kabisa.”
Kutokana na matokeo hayo, timu ya wanasayansi ilibuni kifaa maalum cha kubaini changamoto za kusikia, kinachotumia mchezo wa watoto kupitia headphone. Mtoto anapomaliza kucheza, kifaa hutuma matokeo yanayoonyesha kama ana tatizo au la.
“Kifaa hiki kimetupa tuzo katika makongamano mbalimbali. Kimeonekana ni suluhisho linaloweza kubadilisha maisha ya watoto wengi,” alisema Prof. Mnyanyi.
Katika awamu ya pili, mradi ulipelekwa hadi Ethiopia, ambako ulifanywa kwa kutumia wataalamu kutoka Tanzania. Matokeo yalionyesha asilimia 23.3% ya watoto wana changamoto za kusikia.
Kilichowashangaza watafiti ni kwamba, kwa kutumia wataalamu wa ndani, walifanikiwa kutatua karibu 80% ya changamoto hizo ikithibitisha kuwa tatizo linaweza kushughulikiwa kwa ufanisi bila kutegemea wataalamu kutoka nje.
Prof. Mnyanyi aliitaka serikali kuharakisha uanzishwaji wa kada za kitaalamu kama udiolojia na teknolojia ya hotuba (speech technology) kwa ngazi ya diploma ili kuendana na mahitaji makubwa ya jamii.
“Kwa sasa hakuna hata chuo kimoja nchini kinachofundisha kada ya udiolojia, lakini serikali imeanza hatua za kuanzisha digrii. Hata hivyo, tunahitaji pia kozi za ngazi ya kati ili kuzalisha wataalamu wengi kwa haraka,” alisema.
Mradi wa Ninakusikia umeshirikisha watoto, walimu, wazazi na jamii nzima, na umekuwa ukishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Usikivu Duniani katika mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro na Arusha. Katika matukio hayo, hata watu wazima wamegundua kuwa na matatizo ya kusikia bila wao kujua.
Kwa upande wake, Dkt. Keneth Mlai, bingwa wa masikio, pua na koo kutoka KCMC, alisema tatizo kubwa kwa watoto wengi lilikuwa masikio kuziba kwa nta.
“Nta huzalishwa kwa ajili ya kulinda sikio, lakini ikizalika kupita kiasi au kuchanganyika na uchafu kama mbegu za maharage na mahindi ambayo watoto huchezea, husababisha tatizo kubwa la kuziba masikio,” alisema.
Dkt. Mlai aliongeza kuwa asilimia 60% – 70% ya matatizo ya kusikia yanatokana na mambo yanayoweza kuzuilika, ikiwamo kutopata uchunguzi wa mara kwa mara.
“Wazazi wapeleke watoto kupima masikio, pua na koo mara kwa mara. Maeneo haya yanashirikiana, na usafi ni muhimu ili kuondoa maambukizi yanayoweza kuathiri usikivu,” alisisitiza.
Watafiti wa mradi wanakubaliana kwamba kwa ushirikiano wa serikali, jamii na wadau mbalimbali, Tanzania inaweza kuondoa kabisa changamoto za usikivu kwa watoto na hivyo kuboresha elimu na maisha ya maelfu ya watoto.







