ECO WATER NA SELCOM PESa WAZINDUA MFUMO MPYA WA MALIPO YA CHAKULA KIDIGITALI KWA WANAFUNZI WA VYUO.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Kampuni ya Eco Water kwa kushirikiana na Selcom Pesa imezindua rasmi mfumo wa kisasa wa malipo ya chakula kidijitali ujulikanao kama Eco Plus, utakaowawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kupata huduma ya chakula kwa urahisi, usalama na gharama nafuu.



Akizindua mfumo huo leo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Masoko wa Eco Water, Stanley Magesa, alisema Eco Plus imelenga kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uhakika wa kupata chakula bila changamoto za kutunza pesa taslimu au kuzitumia kwenye matumizi mengine.

Magesa amesema kupitia kadi maalum ya Eco Plus, wanafunzi wataweza kufanya malipo ya chakula katika migahawa iliyo ndani ya vyuo na maeneo jirani bila usumbufu.


“Faida kubwa ya kadi hii ni kuwa fedha inayowekwa ni maalum kwa ajili ya chakula pekee. Huwezi kuitoa kwa matumizi mengine, hivyo inasaidia kusimamia bajeti ya chakula na kumpa mwanafunzi uhakika wa kupata huduma bila wasiwasi,” amesema.


Alifafanua kuwa huduma hiyo sasa inapatikana katika vyuo kadhaa ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), huku maandalizi yakiendelea kuifikisha UDSM, Mzumbe na baadaye vyuo vingine vyote nchini.


Kwa upande wa wazazi na walezi, Magesa amesema “mfumo huo unarahisisha zaidi kwani mzazi anaweza kuweka fedha ya chakula moja kwa moja kupitia huduma ya Selcom Pesa bila kutuma pesa taslimu kwa mwanafunzi”.


Kwa upande wake, Meneja Masoko wa Selcom Pesa, Madata Charles, alisema ubunifu ni kiini cha huduma za Selcom, na ushirikiano na Eco Water umewezesha kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi na watoa huduma vyuoni.


“Selcom Pesa ni akaunti ya kidijitali iliyolenga kupunguza zaidi ya asilimia 60 ya gharama ambazo watumiaji walikuwa wakikumbana nazo kupitia benki au mitandao ya simu,” amesema Mandata.


Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, wanafunzi wa Eco Plus wanaweza kuweka pesa moja kwa moja kupitia Selcom Pesa, kuona miamala yao na kujihakikishia usalama wa fedha zao.


“Pesa ikiwa kwenye kadi haiwezi kuibiwa kama ilivyo kwa pesa taslimu. Pia mfumo huu unarahisisha matumizi na kuongeza usalama wa kifedha kwa wanafunzi,” alisisitiza.


Kwa upande wa watoa huduma ya chakula, Selcom imeeleza kuwa mfumo huo utawawezesha kupata taarifa sahihi za miamala, kuweka kumbukumbu bora za mauzo na kuepuka changamoto za chenchi.



Baadhi ya wanafunzi na wafanyabiashara waliohudhuria uzinduzi huo wamesema Eco Plus itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la ukosefu wa chakula, kukuza nidhamu ya matumizi ya wanafunzi na kuongeza ufanisi kwenye utoaji huduma kwa wafanyabiashara.


Uzinduzi wa mfumo huo unaelezwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post