Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) nchini vimetakiwa kuongeza kasi ya kutoa mafunzo yanayolenga matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hususan akili bandia (AI) na roboti, ili kuwaandaa vijana kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, wakati wa ziara yake katika Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Chemba, ambako pia alikabidhi vifaa vya mafunzo ya ubunifu vitakavyogawiwa katika vyuo 63 vya VETA nchini.
Akizungumza leo Novemba 26,2025 katika ziara hiyo, Mhe. Wanu amesema ni muhimu kwa VETA kuendelea kubuni na kuboresha mitaala ili iendane na mabadiliko ya teknolojia duniani, na hivyo kuwezesha vijana kuwa washindani katika soko la ajira linalobadilika kwa kasi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameutaka uongozi wa chuo hicho kurejesha kozi za muda mfupi zilizowahi kutolewa awali, ikiwemo kozi zinazohusiana na kilimo na ufugaji, ambazo alisema ni muhimu kwa kuendeleza shughuli kuu za uchumi katika Wilaya ya Chemba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyn Nombo, amesema wizara inaendelea kuipa kipaumbele sekta ya ufundi stadi kwa kuijengea uwezo ili izalishe vijana wenye umahiri na ujuzi kulingana na mwelekeo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, toleo la 2023.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassanimefanya kazi kubwa kuboresha miundombinu ya vyuo vya VETA na kuhakikisha kila chuo kinapatiwa vifaa vya kisasa.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo 65 vipya vya VETA nchi nzima ili kukidhi mahitaji ya vijana wanaotaka kupata ujuzi wa ufundi stadi.
Aidha, amesema jumla ya shilingi bilioni 7 zimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya mafunzo katika vyuo hivyo.
Ziara ya Naibu Waziri inalenga kujionea utekelezaji wa majukumu ya VETA, kutathmini mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa, pamoja na kupanga mikakati ya kuendelea kuimarisha ubora wa mafunzo ili kuzalisha wataalamu mahiri watakaoliendeleza taifa.








