UMOJA WA WAZAZI WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUCHOCHEA AMANI BAADA YA VURUGU ZA UCHAGUZI “HOTUBA YA RAIS IMETUGUSA, IMETUTIA FARAJA”


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Sisi kama wazazi, Umoja wa Wazazi Tanzania chini ya Jumuiya ya Chama Cha Mapinduzi, tumepokea kwa mtazamo chanya na wa faraja hotuba ya maelekezo iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo ameonesha dhamira ya dhati ya kutibu taifa na kulinda mustakabali wa vijana wa Tanzania.


Hayo yamesemwa leo Novemba 15, 2025 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Taifa wa Umoja wa Wazazi Tanzania, CDE. Fadhili Rajabu Maganya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na hotuba ya uzinduzi wa Bunge aliyoitoa Rais Samia jana mjini Dodoma.


Akizungumza na wanahabari, Maganya alisema hotuba ya Rais imejaa maelekezo muhimu kwa taifa na imebeba ujumbe mahususi unaogusa maisha ya watanzania wote, hasa katika kipindi hiki ambacho nchi imetoka kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29.


Maganya ameeleza kuwa licha ya kampeni kuendelea kwa amani na utulivu, vurugu zisizotarajiwa zilijitokeza siku ya uchaguzi na kusababisha uvunjifu wa amani, vifo vya baadhi ya wananchi hasa vijana pamoja na uharibifu wa mali za serikali na mali binafsi.


“Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vililazimika kuchukua hatua kudhibiti hali ile. Katika kudhibiti, kulikuwa na watu waliokamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Tumemsikia Mhe. Rais akitoa wito wa dhati, kama mzazi na mlezi wa taifa, kuwataka wajibu wa kusimamia haki uzingatie mizani ya makosa yaliyotendeka,” amesema Maganya.


Maganya ameipongeza serikali kwa kuonesha utayari wa kuleta maridhiano miongoni mwa watanzania, akisema hatua ya Rais kuwataka wahusika kuchuja kesi na kuwaachia huru wale wenye makosa madogo ni ishara ya uongozi wa huruma, busara na umoja.


“Tunaona hatua hii kama mwendelezo wa dhamira ya Rais Samia kujenga taifa lenye mshikamano, heshima, haki na amani. Kama wazazi, tunamuunga mkono na tunampongeza kwa uongozi unaojali watoto wetu na mustakabali wa vizazi,” aliongeza.


Maganya ametumia nafasi hiyo kuwasihi watanzania kuendelea kudumisha amani, kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi, na kuunga mkono juhudi za maridhiano zinazoendelea.



🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post