Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha jina la Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mhe. Mussa Azzan Zungu(CCM), kuwa Spika wa Bunge la 13, akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Dk. Tulia Ackson, ambaye alijitoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Katika uchaguzi uliofanyika jijini Dodoma, Mhe. Zungu alipata kura 378 kati ya kura 383 zilizopigwa, akiwashinda wagombea watano kutoka vyama vingine vya siasa. Uchaguzi huo ulifanyika mbele ya wabunge wateule wa Bunge la 13 baada ya kila mgombea kupewa nafasi ya kujieleza na kuomba kura.
Wagombea waliokuwa wakishindana na Mhe. Zungu ni Veronica Charles (NRA), Anitha Mgaya (NLD), Chrisant Ndege (DP), Ndonge Said Ndonge (AAFP) na Amin Yongo (ADC).
Kabla ya kupiga kura, wagombea hao walieleza dhamira zao za kuliongoza Bunge lenye uwajibikaji, ushirikiano na lenye kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Veronica Charles wa NRA alisema akichaguliwa atalifanya Bunge liwe la usawa na la wananchi, huku akiahidi kuondoa kambi rasmi ya upinzani na kuanzisha kambi ya majadiliano kwa lengo la kuimarisha umoja bungeni. Alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi mwenye mfano wa kuigwa.
Anitha Mgaya wa NLD alisema atahakikisha nidhamu, heshima na utulivu vinatawala mijadala bungeni, huku akiahidi kuwaelimisha vijana kuhusu thamani ya amani na upendo.
Chrisant Ndege wa DP aliahidi kusimamia Bunge lenye uwezo wa kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba, akisisitiza umuhimu wa mihimili mitatu ya dola kufanya kazi kwa ushirikiano na uadilifu.
Ndonge Said Ndonge wa AAFP alitumia falsafa ya neno KIONGOZI kueleza misingi ya uongozi wake, akibainisha kuwa kiongozi anapaswa kukubali kukosolewa, kujua tabia za anaowaongoza, kuonyesha kwa vitendo, na kugawa madaraka kwa usawa.
Kwa upande wake, Amin Yongo wa ADC alisema akichaguliwa, ataweka msisitizo katika kulinda amani, umoja wa kitaifa na Katiba ya nchi.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mhe. Musa Azzan Zungu aliahidi kuliongoza Bunge kwa umoja na mshikamano, akisema atahakikisha linafanya kazi kwa ufanisi katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Aliongeza kuwa atasimamia uhusiano mzuri kati ya Bunge na wananchi, ili hoja zinazojadiliwa ziwaguse moja kwa moja Watanzania.
Kuchaguliwa kwa Mhe. Zungu, ambaye katika Bunge lililopita alikuwa Naibu Spika, ni hatua muhimu katika safari yake ya kisiasa, ikionyesha imani kubwa aliyopewa na wabunge pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).


