BABA LEVO KUFANYA MKUTANO MKUBWA WA SHUKRANI KIGOMA MJINI, AWAHIDI KUWATUMIKIA WANANCHI KWA UADILIFU

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mbunge mteule wa Kigoma Mjini, Clayton Revocatus (Baba Levo), ametangaza kufanya mkutano mkubwa wa shukrani kwa wananchi wa jimbo hilo wiki ijayo, akisema utakuwa ni tukio la kihistoria litakalolenga kuwashukuru wapiga kura kwa imani waliyoonyesha kwake na kueleza vipaumbele vyake vya maendeleo kwa miaka mitano ijayo.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Novemba 8, 2025, jijini Dodoma, Baba Levo amesema mkutano huo utafanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja vya Kigoma Mjini, na utakuwa ni fursa maalum ya kutoa shukrani rasmi kwa wananchi pamoja na kueleza dira yake ya maendeleo itakayolenga kutatua changamoto mbalimbali za wananchi katika sekta za elimu, afya, ajira na miundombinu.


“Mkutano huu ni wa wananchi wangu wa Kigoma Mjini, wamechagua na nina deni kwao. Nitawashukuru rasmi na kuwaeleza vipaumbele vyangu nitakapoanza kazi ya ubunge,” amesema Baba Levo.


“Nilipojisajili niliombwa nitaje mashahidi watakaoshuhudia nikiapishwa, mmoja wao ni Diamond Platnumzpamoja na jamaa zangu wa karibu,” aliongeza.


Akizungumzia siasa za Bunge lijalo, Baba Levo alisema kura yake ya Uspika ataipigia aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge lililopita, Azan Zungu, akimtaja kuwa kiongozi mwenye uadilifu, usawa na uzoefu mkubwa katika uongozi.


Aidha, kwa nafasi ya Naibu Spika, Baba Levo alisema ataunga mkono Daniel Sillo, lakini akasisitiza kuwa yuko tayari kumuunga mkono mgombea mwingine yeyote atakayeshinda kwa maslahi mapana ya Taifa.


Mbunge huyo mteule pia amewapa pole wananchi wote waliopata madhara wakati wa kipindi cha uchaguzi mkuu, akiwataka kuendelea kudumisha amani, upendo na umoja, mambo ambayo alisema ndiyo nguzo za maendeleo ya Kigoma na Tanzania kwa ujumla.



🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post