Na Carlos Claudio, Dodoma📍.
Mbunge mteule wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando, maarufu kama Baba Levo, ameonyesha furaha na shukrani kubwa kwa kufanikiwa kuingia rasmi Bungeni, akiwakilisha wananchi wa Kigoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika tukio hilo maalum lililofanyika siku yake ya kwanza ya kuapishwa, Baba Levo alieleza hisia zake za dhati kwa wale wote waliomsaidia kufikia mafanikio hayo, huku akimtaja Naseeb Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ kama mtu aliyechangia pakubwa kumtoa kwenye maisha ya mtaani na kumfanya aaminike katika jamii.
“Nina furaha sana leo. Familia yangu imefika Bungeni kushuhudia siku yangu ya kwanza. Hii ni hatua kubwa maishani mwangu, na ninamshukuru sana Diamond kwa kuniamini, kunitoa mitaani na kunifanya nione inawezekana kubadilisha maisha yangu,” alisema Baba Levo kwa furaha.
Mbunge huyo mpya aliongeza kuwa ameambatana na mke wake pamoja na mtoto wake Bungeni, ili wawe sehemu ya historia yake mpya ya kulitumikia jimbo la Kigoma Mjini.
Kwa upande wake, Diamond Platnumz, ambaye ni Mkurugenzi wa Wasafi Media na mwanamuziki nyota barani Afrika, alitoa pongezi zake kwa Baba Levo, akisema hatua hiyo ni ushahidi kuwa vijana wanaweza kufanikiwa ikiwa watakuwa na juhudi na kujituma.
“Kile alichokifanya Baba Levo kinatia moyo sana. Kimeonyesha kwamba kila kitu kinawezekana. Vijana wasikate tamaa, waamini katika ndoto zao na wafanye kazi kwa bidii,” alisema Diamond.
Diamond pia aliishukuru Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumwamini Baba Levo na kumpa nafasi ya kugombea ubunge, akisisitiza kuwa hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa vijana wengi nchini.
Baba Levo amemalizia kwa kutoa shukrani kwa wananchi wote wa Kigoma Mjini kwa imani waliyoonesha kwake na kuahidi kufanya kazi kwa bidii, uwazi na uadilifu katika kulitumikia jimbo hilo.
“Naahidi sitawaangusha. Nitahakikisha Kigoma Mjini inasonga mbele na kila kijana anaona matokeo ya kazi yetu,” alisema kwa kujiamini.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.





