Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imewataka Watumishi wa Umma kote nchini kuzingatia sheria, kanuni, taratibu pamoja na mienendo ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, zenye weledi na heshima.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB), Bi. Hilda Kabissa, wakati akifungua kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa maadili na utawala bora kati ya taasisi simamizi za maadili ya utendaji na mamlaka za kitaaluma.
Bi. Kabissa amesema ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya watumishi wa umma kutoa huduma zisizoridhisha ikiwemo kutumia lugha zisizofaa, kudharau utu wa wateja, na kutoa majibu yanayokatisha tamaa.
“Tabia hizi ni kinyume na misingi ya sheria na maadili ya utumishi wa umma. Ni lazima tubadili mtazamo ili kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao,” alisisitiza.
Aidha, amewakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha mafunzo ya maadili yanapewa kipaumbele kwa watumishi wapya na waliopo kazini. Alibainisha kuwa baadhi ya ofisi za umma zimeshindwa kutenga au kutumia ipasavyo fedha za mafunzo ya maadili zilizowekwa kwenye bajeti kupitia Lengo B (kukuza uadilifu na juhudi dhidi ya rushwa).
“Ukosefu wa kipaumbele katika mafunzo haya umechangia kuwepo kwa watumishi wasiokuwa waadilifu na waliokosa weledi wa taaluma, hali inayorudisha nyuma juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa,” alisema.
Vilevile, Kaimu Katibu Mkuu huyo alisisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika utoaji huduma za Serikali, akibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika teknolojia ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kupunguza mianya ya rushwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais – Utumishi, Bi. Felister Shuli, alisema kikao hicho ni utekelezaji wa maazimio ya vikao vya awali vya kubadilishana uzoefu kati ya taasisi husika.
“Kama ilivyoazimiwa mwaka 2023, vikao hivi hufanyika mara mbili kwa mwaka kwa utaratibu wa kubadilishana. Mwaka huu TAKUKURU wameratibu kikao cha tano, na sasa OR-MUUUB ndiyo mwenyeji wa kikao hiki cha sita,” alisema.
Bi. Shuli ameongeza kuwa vikao hivyo ni jukwaa muhimu la kujadiliana changamoto na kubadilishana mbinu za kusimamia maadili ya utendaji na kitaaluma kwa watumishi wa umma.
Kikao kijacho kinatarajiwa kuratibiwa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) mwezi Machi, 2026.








