Dodoma.📍
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Antony Mavunde, ameweka mbele ajenda ya uchimbaji visima kama suluhisho la changamoto ya upatikanaji wa maji safi, akiahidi kutekeleza mikakati ya muda mfupi na mrefu kwa ajili ya wakazi wa Kata ya Ipagala na maeneo jirani, ili kumaliza kabisa tatizo hilo sugu linalowakabili kwa miaka mingi.
Akizungumza na wananchi wakati akifanya kampeni katika kata ya Ipagala iliyopo jimbo la Mtumba Mavunde amesema atachimba visima viwili katika kata ya Ipagala na mtaa wa Bwawani kama hatua ya haraka ya kuwapatia wananchi maji kabla ya utekelezaji kamili wa miradi mikubwa ya serikali.
Ameeleza kuwa kwa sasa, jiji la Dodoma linakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la wakazi kutoka watu 765,000 huku vyanzo vya maji vikiendelea kuwa vilevile tangu mwaka 2010.
Akifafanua zaidi, Mavunde ameeleza kuwa mwaka 2010, mahitaji ya maji kwa siku jijini Dodoma yalikuwa lita milioni 47, huku uzalishaji ukiwa lita milioni 67 kupitia visima vitano vya Mzakwe hivyo kuwepo na ziada ya lita milioni 20 na hakuna mgao wa maji wakati huo.
Hata hivyo, ongezeko kubwa la wakazi kufuatia uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma kumesababisha mahitaji kupanda hadi kufikia lita milioni 149 kwa siku, huku uzalishaji ukiendelea kuwa chini ya kiwango cha lita milioni 79 pekee, hali inayoleta upungufu wa zaidi ya lita milioni 70 kwa siku moja.
Katika juhudi za kupunguza pengo hilo, Mavunde ameeleza kuwa visima vitano vimechimbwa katika Kata ya Nzuguni ambavyo huzalisha lita milioni 7.8 kwa siku. Kwa kuwa mahitaji ya Nzuguni ni lita milioni 3.4 pekee kwa siku, ziada ya maji kutoka visima hivyo itapelekwa Ipagala kwa kuwa ni kata ya pili yenye idadi kubwa ya watu baada ya Nzuguni.
"Tayari mkandarasi amepatikana na kazi ya kulaza mabomba inaanza muda wowote ili kuhakikisha mabadiliko ya upatikanaji maji yanawafikia wananchi wa Ipagala" amesema mavunde
Mavunde ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameridhia utolewaji wa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima vingine 13, na hivyo kufanya jumla ya visima 18 vitakavyosaidia kuhudumia Mji wa Serikali Mtumba na maeneo ya jirani.
Amesema mradi huo mkubwa wa serikali utaondoa utegemezi wa chanzo cha maji kutoka Mzakwe kwa upande wa Ipagala, na badala yake kata hiyo itapata maji kupitia mfumo mpya kutoka Nzuguni.
"Muda si mrefu mtaanza kuona mabadiliko. Maji yapo, fedha zipo, mkandarasi yupo. Kazi iliyobaki ni kulaza mabomba. Lakini kabla ya hapo, mimi mwenyewe nitatatua changamoto zenu kwa kuchimba visima hapa Ipagala," amesisitiza Mavunde.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.






