TSC: HATUA ZA KINIDHAMU ZITAWAKABILI WALIMU WANAOKIUKA SHERIA.


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Walimu wametakiwa kuzingatia sheria na taratibu za utumishi wa umma na kuacha kujihusisha na masuala ya siasa kinyume cha miongozo, vinginevyo hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yao.


Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama, wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani.



Aidha, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Masoud Mruke, amesema maadhimisho hayo yanalenga kutambua na kuenzi mchango mkubwa wa walimu katika kukuza maarifa, maadili na malezi ya vizazi vijavyo.


Amesema pia maadhimisho hayo yana lengo la kuelimisha, kuhamasisha na kuwapa motisha walimu katika utekelezaji wa majukumu yao, sambamba na kuchochea mjadala wa kitaifa na kimataifa kuhusu namna ya kuboresha taaluma ya ualimu na mazingira ya utoaji elimu.


“Tunataka kuchochea mjadala mpana wa kitaifa na kimataifa kuhusu namna bora ya kuboresha taaluma ya ualimu na mazingira ya utoaji elimu,” alisema Prof. Mruke.


Prof. Mruke alifafanua kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Wezesha walimu kuchagua viongozi bora kwa elimu na mafunzo stahiki.”


Amesema kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha walimu kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ili kupata viongozi watakaowezesha maendeleo makubwa katika sekta ya elimu.


Miongoni mwa shughuli zilizoandaliwa ni kutembelea vyombo vya habari kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii, pamoja na maonesho maalum katika viwanja vya Nyerere Square, Dodoma, vinavyoendelea hadi Oktoba 5.


“Katika siku ya kilele, kutakuwa na bonanza kubwa litakalowaleta walimu pamoja kushiriki michezo mbalimbali,” alisema Prof. Mruke.


Siku ya Mwalimu Duniani huadhimishwa kila mwaka Oktoba 5, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1994 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ili kuenzi mchango mkubwa wa walimu katika jamii kitaifa na kimataifa.










🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post