Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendesha warsha ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ustahimilivu katika nyanda kavu za kitropiki, inayotarajiwa kuleta suluhisho endelevu la upatikanaji wa maji safi na salama jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa warsha ya mradi huo jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Kutunza na Kuhifadhi Rasilimali za Maji, Bi Rosemary Rwebugisa, amesema kuwa kwa sasa Mamlaka ya Maji ya Jiji la Dodoma (DUWASA) inazalisha kiasi cha maji ambacho hakitoshelezi mahitaji ya wananchi, hivyo uwepo wa mradi huo ni hatua muafaka katika kutatua changamoto hiyo.
“Kwa sasa uzalishaji wa maji haukidhi mahitaji ya wakazi wa Dodoma, lakini Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuimarisha miradi ya uzalishaji na usambazaji maji ili kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa wakati,” amesema Bi Rwebugisa.
Ameongeza kuwa jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Maji zinaendelea kufanyika kwa kasi, ikiwa ni pamoja na kutafuta vyanzo vipya vya maji na kuboresha miundombinu iliyopo ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya wakazi wa Dodoma.
Kwa upande wake, Prof. Japhet Kashaigili, Mkurugenzi wa Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu wa SUA, amesema warsha hiyo inalenga kuleta suluhisho la kisayansi na kiteknolojia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye nyanda kavu.
“Kupitia utafiti na ushirikiano na wadau mbalimbali, SUA inalenga kusaidia jamii na Serikali kupata njia endelevu za kuhifadhi na kusimamia rasilimali za maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Prof. Kashaigili.
Naye Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Utawala na Fedha), Prof. Amandus Muhairwa, amesema ongezeko la kasi la watu na shughuli za kiuchumi jijini Dodoma limeongeza shinikizo kubwa kwenye rasilimali za maji, jambo linalohitaji mipango madhubuti ya usimamizi.
“Mji wa Dodoma unakua kwa kasi kubwa kutokana na uwepo wa serikali kuu, hivyo tunapongeza Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa juhudi zake za kuhakikisha vyanzo vipya vinapatikana na huduma za maji zinaboreshwa,” amesema Prof. Muhairwa.
Mradi huo unaoratibiwa na SUA unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika sekta ya maji kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora, kuboresha maisha ya wakazi wa Dodoma, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.










