WITO WA KUZINGATIA MAADILI YA UISLAMU WATOLEWA DODOMA.

 


Na Mwandishi wetu, Dodoma.📍


Waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuishi kwa kuzingatia maadili ya dini hiyo na kujiepusha na vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinavyoweza kuharibu taswira nzuri ya Uislamu katika jamii.


Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Msemaji wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Ahmed Saidi, wakati wa uzinduzi wa kongamano la kidawa lililoandaliwa na Taasisi ya Muslim Sisters, kongamano lililolenga kuimarisha maadili mema na mshikamano katika jamii ya Kiislamu.


Sheikh Saidi amesema ni jukumu la kila Muislamu kuhakikisha anakuwa kielelezo cha maadili mema, upendo na uadilifu katika jamii, ili kusaidia kupunguza changamoto za kijamii zinazotokana na kuporomoka kwa maadili.


Taasisi kama hizi zina nafasi kubwa sana katika kujenga jamii yenye maadili mazuri, na ni wajibu wetu kama Waislamu kuunga mkono juhudi hizi,” amesema Sheikh Saidi.


Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wahadhiri mbalimbali wa dini ya Kiislamu akiwemo Sheikh Shams Elmi, Sheikh Kombo Ally Fundi na Sheikh Hassan Mohammadyn, ambao kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha misingi ya dini na kuishi kwa kufuata mafundisho ya Uislamu katika kila nyanja ya maisha.




Awali, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Muslim Sisters, Zainabu Kazimiri, amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kutangaza na kukuza dini ya Kiislamu pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa watu wenye uhitaji bila kujali dini, kabila au jinsia.


Tunataka kuona jamii inayojali, inayoishi kwa amani na inayoheshimu maadili mema. Muslim Sisters itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tunafikia malengo haya,” alisema.



🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.







Previous Post Next Post