REA YATOA ONYO KUHUSU UUZAJI HOLELA WA MAFUTA VIJIJINI, YAANZISHA MKAKATI WA VITUO SALAMA.



Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeonya wananchi wanaojihusisha na biashara ya kuuza mafuta ya petroli na dizeli kwa njia zisizo salama, hasa katika maeneo ya vijijini, kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa inahatarisha maisha yao na mali zao.


Kaimu Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, amesema kauli hiyo jijini Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja huku akisema wakala huo umebaini uwepo wa vibanda na maduka madogo yanayouza mafuta kiholela, ambapo wamiliki huhifadhi mafuta hayo majumbani mwao nyakati za usiku kwa hofu ya kuibiwa jambo ambalo amesema ni hatari kubwa.


Kuna baadhi ya wananchi wamekuwa wakiweka madumu ya mafuta majumbani mwao na hata kulala nayo uvunguni. Hii ni hatari sana, kwani tumeshaona matukio kadhaa ya milipuko ikiwemo nyumba kuungua moto baada ya mtu kuwasha sigara karibu na mafuta hayo,” amesema Mhandisi Olotu.


Amesema kutokana na hali hiyo, REA imeandaa mpango maalum wa kuanzisha vituo vidogo salama vya kuuza mafuta katika maeneo ya vijijini, ili kuwaepusha wananchi na majanga yanayosababishwa na utunzaji holela wa nishati hiyo.


Tukasema, ili kuweza kuwalinda wananchi dhidi ya majanga haya, tuwatengenezee utaratibu rasmi wa kupata vituo vidogo salama vya kuuzia mafuta vijijini,” aliongeza.



Kwa mujibu wa Mhandisi Olotu, REA imetenga mkopo wa Shilingi milioni 133 kusaidia vikundi vya wananchi wa vijijini kuanzisha biashara hiyo kwa usalama zaidi. 


Fedha hizo zitatumika kujenga vituo vidogo vya mafuta na kutoa mtaji wa kuanzia kwa watakaozingatia vigezo vilivyowekwa na wakala huo.


Ameeleza kuwa REA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika nyanja zote kuu za nishati umeme, mafuta na gesi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote, hususan wa vijijini, wanapata huduma bora za nishati.


Tunaamini umeme ni kichocheo namba moja cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Serikali imetupa msukumo mkubwa kuhakikisha maeneo tunayofanyia kazi yanakuwa ya kipaumbele kwa maendeleo ya nchi nzima, amesema.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post