AISHA MADOGA AHAIDI KUONGEZA TIJA KILIMONI NA KUPUNGUZA UKOSEFU WA AJIRA DODOMA.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA), Bi Aisha Madoga, ameahidi kushughulikia changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuongeza tija na thamani ya mazao ya kilimo, hususan zao la zabibu ambalo ni miongoni mwa mazao yanayolimwa kwa wingi katika mkoa wa Dodoma.


Akizungumza katika mikutano ya kampeni zake iliyofanyika katika kata za Mpunguzi na Matumbulu, Bi Madoga amesema ukosefu wa ajira kwa vijana ni kilio kikubwa kinachotokana na mifumo isiyowezesha maendeleo yao kiuchumi.


“Tunahitaji mabadiliko ya kweli katika mfumo wa kiuchumi. Vijana wetu wana nguvu na ari, lakini hawana mazingira rafiki ya kutumia fursa zilizopo. 



Nitahakikisha tunaboresha sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao, hususan zabibu, ili kuunda ajira nyingi zaidi,” amesema Bi Madoga.


Bi Madoga aliahidi kuwa ndani ya siku 100 za kwanza endapo atapewa ridhaa na wananchi wa Dodoma Mjini, atahakikisha kufutwa kwa kodi zote zisizo rafiki kwa sekta ya kilimo, hatua itakayowezesha wakulima na wafanyabiashara kufaidika zaidi na shughuli zao.


Aidha, amesisitiza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wote wanapata bima ya afya bila ubaguzi, ili kila mtu aweze kupata huduma bora za afya bila malipo na kwa usawa.


“Nataka kuona kila Mtanzania anapata huduma bora za afya bila kubaguliwa kwa kipato au nafasi yake. Huu ndio ukombozi wa kweli ninaousimamia,” aliongeza.


Bi Madoga amewataka wananchi wa Dodoma Mjini kumpa ridhaa katika uchaguzi ambao upo mbeleni ili awe sauti ya mabadiliko na maendeleo jumuishi katika jimbo hilo.




🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post