Dodoma.📍
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, ameendelea na kampeni zake katika Kata ya Hombolo Makulu, ambako ameahidi kuendeleza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Hombolo Makulu, Mavunde amesema moja ya kipaumbele chake ni ujenzi wa visima vya maji vitakavyotumika kumwagilia mashamba na kwa matumizi ya nyumbani, huku akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha maeneo yote yanapata maji bila mgao.
Mavunde ameongeza kuwa tayari amezungumza na Mkurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhusu tatizo la upatikanaji wa maji katika eneo la Mayeto, ili kuhakikisha kisima kilichochimbwa kinatumika ipasavyo na maji yanawafikia wananchi wote.
Aidha, Mavunde amezungumzia changamoto ya barabara ya Zepisa A, akibainisha kuwa ingawa daraja kubwa limejengwa, upungufu wa makaravati unasababisha maji kukosa mwelekeo sahihi na hivyo kufanya barabara hiyo kuwa ngumu kupitika hasa nyakati za mvua.
Amesema atahakikisha miundombinu hiyo inaboreshwa ili kuwezesha usafiri na shughuli za kiuchumi kufanyika kwa urahisi.
Katika sekta ya afya, Mavunde ameahidi kujenga nyumba za watumishi wa zahanati zilizopo eneo hilo ili kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kuhusu sekta ya biashara, ameeleza kuwa licha ya vibanda vya soko la Zepisa A kujengwa, bado eneo hilo linahitaji paa ili kulifanya kuwa soko kamili litakaloongeza shughuli za uchumi na kuwapa wafanyabiashara mazingira bora ya kufanya kazi.
Pia amegusia suala la umeme, akisema bado yapo maeneo ndani ya Kata ya Hombolo Makulu ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo, lakini Zepisa A na maeneo jirani tayari yamejumuishwa kwenye mradi wa upanuzi wa umeme vijijini.
Mavunde amewataka wananchi kuendelea kuiamini serikali ya CCM, na kuwapa ridhaa yeye pamoja na Mgombea uraisi kupitia tiketi ya CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan ili waendelee kuongoza jitihada za kuleta maendeleo, akiahidi uongozi unaolenga matokeo na maendeleo kwa vitendo.
🚨Subscribe YOUTUBE CHANNEL Yetu Ya WASHINDI MEDIA.







