“SITADANGANYA, NITASIMAMIA MIRADI ILIYOANZISHWA” - AHMED SHABIBY


Na Carlos Claudio, Gairo, Morogoro.


Mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Gairo mkoani Morogoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ahmed Shabiby, ameahidi kuendelea kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa katika awamu ya sita badala ya kutoa ahadi mpya zisizo na uhakika.


Akizungumza kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Gairo, Shabiby amesema wananchi wa jimbo hilo wanamfahamu kwa kusema ukweli na kutotoa ahadi hewa.


“Maneno ya uwongo sipendi. Kama inawezekana, nitawaambia inawezekana, na kama haiwezekani nitawaambia haiwezekani. Sitaki kudanganya. Nimetoka bungeni na najua ugumu wa kule,” alisema Shabiby.


Alibainisha kuwa kipaumbele chake ni kuhakikisha miradi ya maendeleo iliyopatikana chini ya awamu ya sita inakamilika na kuwanufaisha wananchi. 


Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na ule mkubwa wa maji wa Chagongwe wenye thamani ya shilingi bilioni 21.4 unaohudumia vijiji zaidi ya 20 ikiwemo Muheza, Ititu, Kisitwi, Ikenge, na Rubeho.


Shabiby pia alitaja mradi wa maji wa Masenge wenye gharama ya bilioni 8.995 ambao sasa una vyanzo vinne vya maji, pamoja na mradi wa Gairo mjini wa kuchuja chumvi kutoka visimani unaochuja lita milioni 200 kwa siku, ambao alidai ni wa kipekee nchini.


Katika upande wa uchumi na ajira, mgombea huyo aliahidi kutoa mikopo ya pikipiki 3,000 kwa vijana wa jimbo hilo ili kuwawezesha kuongeza kipato na kuendeleza shughuli za kilimo.




Aliongeza kuwa sekta za elimu na afya zimeimarika, akitaja shule mpya, vyoo vipya, na huduma za afya zilizopelekwa hadi vijijini zikiwa na magari ya huduma ya dharura.


Akizungumzia miundombinu, Shabiby amesema barabara za lami zikiongozwa na kipande cha Lubeho- Nongwe zitaendelea kujengwa, huku akieleza kuwa miradi mingine amekuwa akichangia binafsi kuchonga barabara na kuweka madaraja ili wananchi wa Gairo wasikwame.


Shabiby amewataka wananchi kutohukumu mapema kwa kudhani yeye pamoja na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan watashinda bila kura zao, akisema,

“Nipo hapa kufanikisha vyote. Msije mkajidanganya kwamba nitapita bila kupiga kura. Nawaomba kura zenu nyingi ili tuendelee na maendeleo.”


Kauli hiyo ilipokelewa kwa shangwe na vigelegele, huku wananchi wakimhakikishia mshikamano katika safari ya maendeleo ya Gairo.








🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post