JENESTA MALINGO AOMBA RIDHAA YA ZUZU, AAHIDI MAJI, ELIMU NA UCHUMI IMARA.


Na Carlos Claudio, Dodoma. 


Mgombea udiwani wa Kata ya Zuzu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi. Jenesta Malingo, amewataka wananchi wa kata hiyo kumpa kura ili aweze kuwawakilisha kwa ujasiri katika Baraza la Madiwani, akiahidi kutatua changamoto za maji, kuboresha elimu na kuinua uchumi wa wananchi.


Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Zuzu, Bi. Malingo alisema ilani ya CCM 2025–2030 imetoa mwelekeo thabiti wa maendeleo ambao utaigusa moja kwa moja kata ya Zuzu kupitia miradi mikubwa ya maji na mikopo kwa wananchi.


Ndugu wananchi, naombeni kura zenu kwa CCM ili niende kwenye Baraza la Madiwani nikasimame kidedea kuitetea kata yetu ya Zuzu. Bahati nzuri, ilani yetu ya CCM 2025–2030 imetuletea miradi mbalimbali inayogusa moja kwa moja Zuzu. Kwenye upande wa uchumi, tunapaswa kuinuka. Zipo fedha za mikopo ya asilimia 10, nitasimama kidete kuhakikisha vijana, akinamama na watu wenye ulemavu wanapata mikopo bila riba na bila upendeleo, alisema Malingo.


Aidha, Malingo alisisitiza kwamba tatizo la maji limekuwa changamoto kubwa katika mitaa yote ya kata hiyo na akawahakikishia wananchi kuwa CCM imepanga miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi utakaounganisha Zuzu na Nala.

Tunaamini mradi huu utatuacha salama na tutamaliza kabisa shida ya maji katika kata yetu,” aliongeza.


Katika sekta ya elimu, Malingo alisema changamoto ya umbali mrefu kwa wanafunzi wa sekondari ni kubwa na inaleta hatari kwa watoto. 


Aliahidi kushirikiana na baraza la madiwani kuhakikisha shule ya sekondari ya Chididimo inakamilika ndani ya kipindi cha miaka mitano.


Watoto wetu kutoka Soweto na Chididimo wanatembea zaidi ya kilomita 8 kwenda na kurudi kila siku. Hali hii siyo salama. Nitaenda kusimama kidete kuhakikisha shule ya Chididimo inakamilika ili watoto wetu wapate elimu karibu na makazi yao,” alisema.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Bw. Shaban Shaban, alimuelezea Malingo kama kiongozi kijana mwenye maono na ari ya maendeleo.


“Jenesta ni miongoni mwa vijana wetu adhimu. Amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na wananchi na kutoa ushauri juu ya maendeleo ya kata ya Zuzu. Tunamuamini kwa uchungu na thamani anayoweka kwenye maendeleo ya jamii,” alisema Shaban.


Wananchi waliohudhuria mkutano huo walionekana kuridhishwa na ahadi na maono ya mgombea huyo, wakisema ana historia ya kushiriki maendeleo ya jamii na kuonyesha ujasiri wa uongozi hata kabla ya uteuzi wake.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post