NALA YAKONGA MIOYO: MAMIA WAHUDHURIA UZINDUZI WA KAMPENI, LEONARD ATOA AHADI ZA MAENDELEO KWA WAKAZI.


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni uliofurika mamia ya wananchi wa Kata ya Nala, Dodoma, Mgombea Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Leonard Alexander, amewahakikishia wakazi wa eneo hilo maendeleo makubwa endapo watampa ridhaa ya kuendelea kuliongoza eneo hilo.


Akizungumza kwa unyenyekevu mkubwa, Leonard alisema ni muhimu kuangalia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne hadi mitano iliyopita kabla ya kuzungumza kuhusu mipango ya miaka ijayo. 


Alieleza kuwa Nala imenufaika pakubwa na uwekezaji wa serikali, akitaja ujenzi wa Ring Road wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 250, ambao umewawezesha wananchi kupata huduma za usafiri wa uhakika na kuchochea uchumi wa eneo hilo.


Katika sekta ya elimu, Leonard alibainisha ujenzi wa shule mpya mbili Chisegu na Kibaoni ambazo zitapunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu. Aidha, aliahidi kusimamia ujenzi wa madarasa zaidi na kuhakikisha elimu bora inaendelezwa, huku akisisitiza kwamba ajira zitakazotokana na viwanda vipya kama kiwanda cha mbolea, saruji na bia zitawanufaisha wakazi wa Nala kwanza.


Sekta ya afya nayo haikuachwa nyuma. Leonard alisema, "Tuna madaktari bingwa na hospitali ya wilaya iliyoimarika, pamoja na kituo kikubwa cha afya kinachoendelea kujengwa. Huduma hizi zimepunguza mateso ya kina mama na watoto."


Aliongeza kuwa ataendelea kupigania mikopo ya vijana, kina mama na walemavu ili kuwawezesha kiuchumi. Kuhusu migogoro ya ardhi, aliahidi kusimamia haki za wananchi na kuhakikisha hakuna anayepunjwa katika mchakato wa umiliki wa viwanja.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Charles Mamba, aliwataka wananchi waendelee kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa mafanikio kama ujenzi wa barabara ya pete na uwepo wa makao makuu ya serikali ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya maendeleo.



Aidha, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nala, Zabron Kusena, aliwapongeza wananchi kwa mwitikio mkubwa na kueleza kuwa mkutano mwingine mkubwa zaidi utafanyika tarehe 25 Chihoni, ukiwahusisha pia wabunge na wasanii mbalimbali.


Wananchi waliokuwepo walimpongeza Leonard kama kiongozi kijana anayejitambua na kupendwa na jamii yake, huku wengi wakisema kuwa Nala ipo kwenye njia sahihi ya kukombolewa kimaendeleo.












🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post