GSK SECURITY SERVICES YATOA WITO: “SALIMISHE SILAHA KWENYE JESHI LA POLISI, LINDA AMANI YETU”

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Kampuni ya ulinzi ya GSK Security Services, yenye makao makuu jijini Dodoma, imewataka wamiliki wa makampuni ya ulinzi nchini Tanzania kuhakikisha wanazingatia kikamilifu sheria na taratibu za usalama, ikiwemo kusalimisha silaha za moto walizo nazo kinyume cha sheria kwa Jeshi la Polisi.


Akizungumza na washindi Media , Mkurugenzi wa GSK Security Services, Goodluck Sadick Kinyero, alisema kumekuwa na baadhi ya makampuni yanayohazimisha silaha kwa makampuni mengine badala ya kuzisalimisha, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria na kinaweza kuhatarisha usalama wa raia.


“Tunawasihi wenzetu waliokata tamaa kuendesha makampuni yao au kushindwa kuendelea, wasizihamishie silaha hizo kwa makampuni mengine. 


Silaha ni mali ya serikali, na Jeshi la Polisi limeelekeza wazi kwamba zirejeshwe kuanzia tarehe 1 hadi 30 Septemba. Tukio kinyume na hilo litakumbana na ahatua kali za kisheria,” alisema Kinyero.


Aidha, Kinyero amesisitiza kuwa GSK Security Services imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Jeshi la Polisi na mamlaka husika ili kuhakikisha sekta ya ulinzi binafsi inabaki salama na yenye ufanisi.


Kampuni hiyo iliyoanzishwa tarehe 31 Juni 2022, imeweza kutoa ajira kwa zaidi ya vijana 130 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dodoma, Tabora, Manyara, Dar es Salaam na Arusha. 


Kinyero alisema ajira hizo zinatolewa kwa vijana wa Kitanzania waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) au mgambo, ili kuhakikisha huduma ya ulinzi inatolewa kitaalamu na kwa ufanisi.


“Sisi ni kampuni ya kisasa, tofauti na makampuni mengine. Tunazingatia mafunzo, umri na uwezo wa kimwili wa walinzi wetu. Kauli mbiu yetu ni ‘Usalama wa Mali Zako, Karibu Tukuhudumie’, na tumedhamiria kuendelea kulinda watu binafsi, taasisi za serikali na mashirika mbalimbali,” aliongeza Kinyero.


GSK Security Services imesajiliwa rasmi kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni ya Ulinzi ya Mwaka 2022 na ina matawi katika mikoa yote nchini. 


Mkurugenzi huyo aliishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kwa ushirikiano unaoendelea, akibainisha kwamba ulinzi wa raia na mali zao hauwezi kufanikishwa bila mshikamano wa karibu kati ya makampuni binafsi na vyombo vya dola.


Kinyero alihitimisha kwa kusisitiza kuwa ulinzi ni jukumu la pamoja, “Jeshi la Polisi haliwezi kufanya kazi hii peke yake. Tushirikiane kuhakikisha tunapunguza au kumaliza kabisa uhalifu nchini. Makampuni yote ya ulinzi yaheshimu maelekezo ya serikali kwa manufaa ya taifa zima.”












🚨Full VIDEO inapatikana kwenye Instagram Page yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post