“MRADI WA TUINUKE PAMOJA WA AGA KHAN FOUNDATION WAINUA WANAWAKE NA JAMII”



Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


Mwenyekiti wa Youth Ambassador of Hope Unity Leadership, Joshua Sebastian John, amepongeza juhudi za Aga Khan Foundation kupitia mradi wa Tuinuke Pamoja kwa mchango wake mkubwa katika kuinua wanawake na makundi yenye kipato cha chini, hususan katika wilaya za mkoa wa Dodoma.



Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya siku mbili iliyoanza Septemba 9 na kumalizika leo, Septemba 10, 2025, Joshua amesema mafunzo hayo yamewapa nafasi ya kutoa mapendekezo na maoni yatakayosaidia kubaini vikundi vinavyostahili ruzuku isiyo na riba, ambayo inalenga kuwawezesha kiuchumi na kupunguza unyanyasaji wa kijinsia.


“Tumepokea mwaliko kutoka Aga Khan Foundation na kupitia warsha hii tumejifunza mengi. Tumetoa mapendekezo yatakayowezesha taasisi kuinua wanawake na makundi yenye kipato cha chini. 

Hii ni fursa muhimu ya kuwapa wanawake uwezo wa kupaza sauti zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” alisema Joshua.



Kwa upande wake, Rubengo Rubengo, Mratibu wa mradi wa Tuinuke Pamoja katika wilaya ya Kondoa, alisema mpango huo unalenga kuimarisha usawa wa kijinsia na kuinua uchumi wa wanawake. 


Mradi huo, ambao unatekelezwa kwa miaka mitatu, ulianza Kondoa na Chemba na sasa umeenea hadi Chamwino, Bahi na Dodoma Mjini.


“Mradi umejikita kwenye jamii zenye uhitaji mkubwa na changamoto za ukatili wa kijinsia. Tunashirikiana na viongozi wa jamii, maafisa maendeleo na wadau mbalimbali kuhakikisha kinamama wanawezeshwa kiuchumi na kijamii. 


Lengo letu ni kuhakikisha tunakusanya nguvu za pamoja ili kufikia usawa wa kijinsia,” alisema Rubengo.


Shamira Ibrahim, Mweka Hazina wa kikundi cha Kondoa Women, alieleza kuwa mradi umeleta mabadiliko makubwa:



“Tumenufaika sana. Kupitia elimu tuliyopewa, jamii sasa imeanza kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia, na hata viongozi wa dini wamekuwa mstari wa mbele katika kuibua kesi hizi. Changamoto bado zipo, hasa upungufu wa rasilimali na ushirikiano mdogo kutoka baadhi ya viongozi wa serikali, lakini tunaamini elimu endelevu italeta matokeo makubwa.”


Warsha hiyo pia ilisisitiza umuhimu wa elimu vijijini kuhusu kupinga mimba na ndoa za utotoni, huku vikundi vitakavyopokea ruzuku vikitakiwa kuanzisha miradi endelevu inayoweza kubadilisha maisha ya wanajamii.


Taasisi ya Aga Khan Foundation na wadau wengine wa maendeleo wametajwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kuondoa ukandamizaji wa kijinsia na kuweka msingi wa maendeleo jumuishi katika jamii za mkoa wa Dodoma.


🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post