Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala katika Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais – Utumishi, Kamishna Mwandamizi wa Polisi Ibrahimu Mahumi, ametoa wito na maagizo kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya kuhakikisha wanaandaa na kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya mafunzo ya makatibu tawala.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa ufungaji wa mafunzo ya siku tano ya Menejimenti na Itifaki za Vikao na Mikutano kwa makatibu, yaliyoratibiwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Mahumi ameeleza masikitiko yake kwamba kati ya halmashauri 184, ni 55 pekee ndizo zilizowakilisha makatibu tawala wao kwenye mafunzo hayo.
“Hii ina maana zaidi ya halmashauri 120 hazikuleta watu. Naomba hii iwe fundisho. Bajeti ni maandalizi, tenga fedha kwa ajili ya mafunzo kama haya. Chuo cha Utumishi wa Umma kinafanya kazi kubwa, lakini lazima tupange mapema na tuwasilishe mipango yetu kwa Katibu Mkuu Mtumishi kabla ya utekelezaji,” alisema Mahumi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa usiri wa taarifa za serikali, hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi.
“Usiri ni sehemu muhimu ya utendaji wa serikali.
Taarifa ndogo unayoiona ya kawaida inaweza kuwa hatari mikononi mwa mtu asiyehusika. Tuelimishane na tuwe chachu ya mabadiliko kwa wengine,” aliongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mafunzo ya Watumishi wa Umma, Fadhili Mtinda, amesema mafunzo hayo yamekuwa jukwaa la kipekee la kubadilishana uzoefu na kupata mbinu mpya.
Washiriki walijengewa uwezo katika uandishi wa muhtasari, uandaaji wa taarifa za vikao, matumizi ya TEHAMA na akili bandia (AI), pamoja na elimu ya fedha, uwekezaji na udhibiti wa hisia.
Mtinda alibainisha kuwa chuo hicho kimepokea na kukubali ombi la kuendesha mafunzo mengine kwa kada mbalimbali za utumishi wa umma.
“Tunashukuru kuona washiriki wamepata maarifa yatakayoongeza thamani katika utendaji wao wa kila siku na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dkt. Sayuni Nasari, aliyetoa somo la akili hisia, amesisitiza umuhimu wa kujitambua na kudhibiti hisia katika maeneo ya kazi.
“Hisia zina athari kubwa kuliko akili ya kawaida. Ukijua namna ya kuzitafsiri na kuzidhibiti, ni rahisi kufanya maamuzi sahihi na kuboresha mahusiano kazini,” alisema.
Mafunzo haya yametajwa kama hatua muhimu katika kuinua ufanisi wa makatibu tawala na kuboresha utendaji katika halmashauri za wilaya nchini.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.








