COOP BANK NA NIC WASHIRIKIANA KUINUA SEKTA YA KILIMO KWA HUDUMA ZA BIMA VIJIJINI


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Benki ya Ushirika (Coop Bank) na Shirika la Bima la Taifa (NIC) leo wamesaini mkataba wa kibiashara jijini Dodoma, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia huduma za bima mahsusi kwa wakulima na vyama vya ushirika nchini.



Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Abdi Mkeyenge, amesema shirika hilo limejipanga kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uwekezaji wa ada za bima kwenye benki za biashara nchini.


“Benki hii ikiwa na nguvu basi vyama vyenyewe vitakuwa na nguvu na wamiliki watafaidika, lakini pia tunamwangalia mkulima wa chini ambaye anatakiwa kuinuliwa. Sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa nchi yeyote, hasa sisi ambao tumebarikiwa eneo kubwa la kufanya kilimo,” alisema Mkeyenge.


Amefafanua kuwa NIC inatoa huduma za bima za maisha, mali, ajali na majanga, pamoja na bima za credit life ambazo hulinda dhidi ya upotevu wa fedha. Alisisitiza kuwa ushirikiano na Coop Bank ni mkakati wa “kubakisha uchumi ndani ya nchi” kupitia uwekezaji wa ndani.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank, Godfrey Ng’urah, amesema ushirikiano huo unalenga kujibu changamoto za muda mrefu za ukosefu wa bima mahsusi kwa sekta ya kilimo.


“Tutaangazia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na mnyororo wa thamani wa kilimo biashara. Tunaingia na bima zitakazojibu ukosefu wa bima katika sekta ya kilimo biashara. Kwa kushirikiana na NIC, tutatoa huduma hizi kwa niaba yao kwa wateja wetu,” alisema Ng’urah.


Aliongeza kuwa zaidi ya asilimia 65–70 ya Watanzania wanaishi vijijini na uchumi wao unategemea kilimo, hasa kupitia vyama vya ushirika. 


Aidha ametaja kuwa kuna zaidi ya vyama vya msingi vya kilimo 6,000 vyenye wanachama milioni 8, pamoja na vyama vya fedha (SACCOS) karibu 2,000 vyenye wanachama milioni 2.


Ng’urah amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya maendeleo ya benki za sekta ya ushirika, pamoja na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, wanahisa wa benki na vyama vya ushirika vinavyomiliki zaidi ya asilimia 51 ya Coop Bank.


Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza wigo wa huduma za kifedha na bima hadi kufikia zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaojihusisha na kilimo vijijini, hatua inayotajwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wa kilimo nchini.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post