MKOA WA MBEYA WAANZA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI, WANANCHI WATAKIWA KUTUMIA MFUMO WA NAPA KIDIGITALI

 


Na Carlos Claudio, Mbeya.


Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe. Solomoni Itunda, amezindua rasmi zoezi la uhakiki wa taarifa za anwani za makazi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, akiwataka viongozi na wananchi kushirikiana kuhakikisha mfumo wa kidijitali wa anwani za makazi (NaPA) unafanya kazi kwa ufanisi na endelevu.


Akizungumza katika ukumbi wa Loleza Girls Secondary School, Mhe. Itunda amesema kabla ya zoezi hilo kuanza, viongozi wa mitaa wamepatiwa mafunzo maalum ili kuwajengea uwezo wa kusimamia na kutekeleza mfumo huo. 


Amesisitiza kuwa mafunzo hayo hayapaswi kubaki kwa viongozi pekee, bali yatumike kuwasaidia wananchi kuelewa na kutumia mfumo huo ipasavyo.


Niwaombe wote mtakaopata mafunzo haya mtumie vyeo vyenu na uelewa mliopata kusaidia wananchi. Mfumo huu ni msingi wa maendeleo na utumike kama ulivyokusudiwa, alisema Itunda.


Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa matumizi ya anwani za makazi ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya 2050 na ajenda ya kimataifa ya 2030 kuhusu malengo ya maendeleo endelevu. 


Ameongeza kuwa mfumo imara wa anwani ni kichocheo cha uchumi wa kidijitali na maendeleo ya kijamii.


Aidha, amewaagiza watendaji wa halmashauri na mitaa kuhakikisha zoezi hili linaendelea hata baada ya muda rasmi wa uhakiki kumalizika “Msisitegemee kusikia kuwa mmekoma kufikisha taarifa baada ya siku za zoezi hili kumalizika. Zoezi la uhakiki ni endelevu,” alisisitiza.


Mhe. Itunda pia aliitaka TARURA, TANROADS na halmashauri kushirikiana kuhakikisha barabara zote za Jiji la Mbeya zina nguzo za majina, jambo alilosema litaboresha zaidi mfumo wa utambuzi wa makazi na utoaji huduma.



Kwa upande wake, Bi. Josephine Mwaijande, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara husika, alisema kuwa serikali tayari imeunganisha mfumo wa NaPA na mifumo mingine ya utoaji huduma za kijamii. 


Hii ni pamoja na huduma zinazohitaji kufikishwa majumbani na taratibu za mikopo ya elimu ya juu, ambazo sasa zinahitaji barua ya utambulisho inayotolewa kidijitali kupitia NaPA.


Amebainisha kuwa kufikia 21 Septemba 2025, jumla ya barua 668,000 za anwani za makazi kidijitali zimetolewa nchi nzima, huku Jiji la Mbeya likiwa na maombi 14,325, yote yakiwa yameshughulikiwa kikamilifu.


Dhamira ya serikali ni kila mwananchi ajue na atumie anwani yake ya makazi katika kupokea huduma. Hii ni hatua muhimu ya kuboresha utoaji huduma na mipango ya maendeleo,” amesema Bi. Mwaijande.


Serikali imesisitiza kuwa mfumo wa NaPA ni daftari rasmi la kidijitali kwa mitaa na vijiji, na kila mtendaji ana jukumu la kuhakikisha kila mkazi katika eneo lake amesajiliwa na taarifa zake ziko sahihi. Mfumo huu unatarajiwa kuongeza ufanisi katika kupanga mipango ya maendeleo, uchumi wa kidijitali, na maisha bora kwa wananchi.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post