ZOEZI LA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI MBEYA KUVUKA NYUMBA KWA NYUMBA KUANZIA ALHAMISI


Na Carlos Claudio, Mbeya.


Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza kuwa kuanzia Alhamisi, Septemba 25, zoezi la uhakiki na uhuishaji wa taarifa za anwani za makazi katika Jiji la Mbeya litaendelea kwa kupita nyumba kwa nyumba.


Tangazo hilo limetolewa na Afisa Tehama wa Wizara hiyo, Bi. Rehema Chillo, katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la uhakiki lililofanyika katika ukumbi wa Loleza Girls Secondary School.


Bi. Rehema amesema lengo ni kuhakikisha taarifa zote za anwani zinasahihishwa na kuboreshwa ili mfumo wa kidijitali wa NaPA uwe sahihi na wa kuaminika.


Baada ya mafunzo haya, tarehe 25 siku ya Alhamisi tutaanza kupita nyumba kwa nyumba kuhakiki na kuhuisha taarifa za anwani za makazi. Zile zilizo na makosa zitarekebishwa, na wale ambao hawakupata anwani awali watapatiwa anwani mpya na taarifa zao zitaingizwa kwenye mfumo wa kidijitali wa NaPA,”amesema.


Amefafanua kuwa mafunzo kwa watendaji wa mitaa, kata na wenyeviti yanaendelea kwa siku mbili ili kuhakikisha timu zote zina uelewa wa kutosha.


Tupo hapa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kwa kazi ya kuhakiki taarifa za anwani katika mitaa na kata zote. Kesho ni siku ya pili ya mafunzo haya, tukiwajengea uwezo watendaji wa kata na mitaa,” ameongeza.


Kwa mujibu wa takwimu za awali, mfumo wa NaPA ulikusanya takribani anwani 481,000 katika Jiji la Mbeya, lakini idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka baada ya zoezi jipya kukamilika, kutokana na maeneo ambayo hayakufikiwa awali.


Bi. Rehema ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kamili kwa watendaji watakaopita katika makazi yao, kwa kutoa taarifa sahihi zinazohitajika.


Kama mtu hatakutwa nyumbani, tunaomba aache taarifa muhimu kama namba ya kiwanja, jina la mmiliki, namba ya simu, NIDA, pamoja na taarifa za wategemezi kama mke, mume, watoto, ndugu au wapangaji. Mfumo huu ni muhimu kwa kila mmoja wetu kwani unarahisisha utoaji huduma na kuhakikisha huduma zinamfikia mhusika ipasavyo, amesisitiza.



Wizara imeeleza kuwa mfumo wa anwani za makazi unaleta manufaa makubwa kwa wananchi wote na wageni, kwa kuwa unawezesha kupata huduma haraka, kufahamu eneo husika, na kuboresha mipango ya maendeleo.


Zoezi hili linaendelea kuwa sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuboresha huduma za kijamii, huku likitarajiwa kuongeza usahihi wa taarifa na ufanisi katika utoaji wa huduma mbalimbali nchini.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post