Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali imewataka makatibu wa kamati za halmashauri nchini Tanzania bara kuhakikisha wanajiepusha na matumizi yasiyo salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kulinda usiri na usalama wa taarifa muhimu zinazojadiliwa kwenye vikao vya mamlaka za Serikali za Mitaa.
Agizo hilo limetolewa jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya Menejimenti na Itifaki za Vikao na Mikutano kwa makatibu hao, yaliyoratibiwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Utumishi, Mkurugenzi wa Uendelezaji Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma, Leila Mavika, alisema usiri wa taarifa ni nguzo muhimu inayoiwezesha serikali kutekeleza mipango yake ipasavyo.
“Mada hizi zimeandaliwa mahsusi kwa ajili yenu. Ninaamini zitawajengea maarifa mapya na mbinu za kisasa zitakazoongeza ufanisi katika utumishi wa umma,” alisema Mavika.
Aliongeza kuwa wizara itaendelea kusimamia sera na kutoa miongozo ya kuhakikisha mafunzo kama hayo yanaendelea kutolewa kwa utaratibu endelevu.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma – Taaluma, Tafiti na Ushauri, Dkt. Hamisi Amani, alisema mafunzo hayo yamelenga kuongeza uwezo wa makatibu katika maandalizi, uendeshaji na ufuatiliaji wa maamuzi ya vikao vya serikali za mitaa.
Naye Meneja wa Mafunzo ya Watumishi wa Umma, Fadhili Mtinda, alisema tafiti zinaonesha viwango vya uandishi wa mihutasari bado haviridhishi, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea ujuzi wa kitaalamu na uzoefu katika kuandaa nyaraka sahihi na zenye viwango.
Mwenyekiti wa Umoja wa Makatibu wa Vikao vya Halmashauri Tanzania bara, Ismail Rashid, alitumia nafasi hiyo kuomba serikali kutoa waraka mpya unaoeleza masuala ya kada yao, ikiwemo kuboreshwa kwa viwango vya mishahara ili kuendana na kada nyingine za utumishi.
Aidha, washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Grace Gambadu, Katibu wa Vikao Halmashauri ya Musoma, walisema wamepata mwongozo mpya wa kutumia mifumo ya TEHAMA ili kupunguza matumizi ya karatasi na kuongeza ufanisi wa vikao.
Naye Frank Msuya kutoka Halmashauri ya Babati alisema mafunzo hayo yatasaidia makatibu kutoa mchango mkubwa katika kuboresha uendeshaji wa vikao, uandaaji wa ripoti na kufuata kanuni kwa usahihi zaidi.
Kwa siku tano, washiriki watafundishwa mada mbalimbali ikiwemo uandishi wa mihutasari, maandalizi ya maazimio, matumizi ya TEHAMA, elimu ya fedha na uwekezaji, uongozi binafsi, mbinu za kudhibiti hisia pamoja na usiri na usalama wa taarifa za serikali.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.










