Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Dodoma Mjini, Paschal Chinyele, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi wa kata za pembezoni, hususan upatikanaji wa maji na miundombinu ya afya, iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge.
Akizungumza leo, Septemba 5, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika kata ya Chang’ombe, Chinyele alisema kero kubwa inayowakabili wakazi wa jimbo hilo ni ukosefu wa maji ya uhakika, jambo linalosababisha wananchi kutumia muda na gharama kubwa kutafuta huduma hiyo muhimu.
“Jimbo letu limekuwa na changamoto kubwa ya maji. Nikichaguliwa kuwa mbunge wenu, nitasimamia uchimbaji wa visima vipya na ujenzi wa matenki makubwa ya kuhifadhia maji kwenye maeneo ya vilima ili kuhakikisha huduma hii inasogezwa karibu na wananchi,” alisema Chinyele huku akishangiliwa na umati wa wakazi wa Chang’ombe.
Aidha, alisema atahakikisha kila mwezi anatembelea angalau kata mbili au tatu kusikiliza kero za wananchi na kushirikiana na mamlaka husika katika kuzitafutia ufumbuzi.
“Nataka wananchi wa Dodoma wapate huduma bora za maji na afya. Nitaweka nguvu kubwa kuhakikisha hospitali na zahanati zetu zinakuwa na vifaa tiba na dawa za kutosha,” aliongeza.
Uzinduzi huo wa kampeni ulivuta mamia ya wakazi wa kata ya Chang’ombe, waliyojitokeza kwa wingi kumuunga mkono na kuahidi kushirikiana naye kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi ujao wa ubunge.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.





