KIMBISA: WANACHAMA CCM WASUSIE MAKUNDI, WASHIRIKIANE KUPATA USHINDI



Carlos Claudio, Dodoma.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, amewataka wanachama na wagombea ambao hawakupitishwa katika mchakato wa kura za maoni kutojiondoa au kukata tamaa, bali waendelee kushirikiana na chama kwa ajili ya ushindi wa jumla.


Akizungumza leo Septemba 5, 2025 katika uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Paschal Chinyele, katika kata ya Chang’ombe, Kimbisa amesema siasa ni mchezo wa uvumilivu na mshikamano, hivyo makundi yaliyoundwa wakati wa kusaka uteuzi yafutwe mara baada ya mchakato huo kumalizika.


Katika maisha ya siasa, kosa kubwa ni kususia chama. Vyeo vipo vingi na nafasi za teuzi hazijaisha. Naomba ndugu zangu mvunje makundi. Wakati wa kutafuta kura makundi hayaepukiki, lakini yakishamalizika, tuungane pamoja kwa ajili ya chama chetu, alisema Kimbisa.


Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Dodoma Mjini, Paschal Chinyele, ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi wa kata za pembezoni, hususan upatikanaji wa maji na miundombinu ya afya.


Alisema jimbo hilo limekuwa na changamoto kubwa ya maji, hivyo akichaguliwa atahakikisha visima vipya vinachimbwa na matenki makubwa ya kuhifadhia maji yanajengwa kwenye maeneo ya vilima ili kusogeza huduma karibu na wananchi.


Kila mwezi nitatembelea angalau kata mbili au tatu ili kusikiliza changamoto za wananchi na kushirikiana na mamlaka husika kuzitatua. Nataka kuhakikisha wananchi wa Dodoma wanapata huduma bora za maji na afya,” alisema Chinyele.


Naye mgombea udiwani wa kata ya Chang’ombe kupitia CCM, Bakari Fundikila, alisema kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya miradi kutokamilika, ikiwemo jengo la mama na mtoto pamoja na barabara ambazo huharibika wakati wa mvua.


Aliahidi kushirikiana na wananchi na serikali kukamilisha miradi hiyo muhimu ili kuinua ustawi wa wakazi wa kata hiyo.


Uzinduzi huo wa kampeni ulivuta mamia ya wakazi wa kata ya Chang’ombe ambao walijitokeza kwa wingi kumuunga mkono mgombea wao na kuahidi kushirikiana kuhakikisha CCM inapata ushindi katika uchaguzi ujao.


🚨Subscribe YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post