Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Bi. Aisha Madoga, amewataka wakazi wa Dodoma kumchagua kiongozi atakayewakilisha na kusimamia masilahi ya wananchi bungeni badala ya kushabikia serikali.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Soko la Majengo, Bi. Madoga alisema nafasi ya mbunge ni ya kuwasemea wananchi bungeni na kuibua changamoto zinazowakabili.
“Mna wajibu wa kuchagua mtu ambaye akiingia bungeni ataenda kuzungumza shida zenu, siyo kwenda kuitetea serikali. Mbunge kazi yake ni kuwa mwakilishi wa wananchi,” alisema Bi. Madoga huku akishangiliwa na umati wa wananchi waliokusanyika sokoni hapo.
Alifafanua kuwa jimbo la Dodoma Mjini lina zaidi ya wapiga kura laki mbili, na haiwezekani wote kuingia bungeni kwa pamoja. Hivyo, wananchi wanapaswa kumchagua mtu sahihi atakayebeba sauti ya kila mmoja wao.
“Ingekuwa inawezekana tungeingia wote bungeni, lakini haiwezekani. Ndiyo maana tunachagua mtu mmoja akaendelee kuwasemea wananchi wote wa Dodoma Mjini,” aliongeza.
Bi. Madoga pia aliwahimiza wananchi kutambua umuhimu wa kura zao na kuzitumia ipasavyo ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
🚨VIDEO Inapatikana Kwenye YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.






