WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YATOA ELIMU YA UCHAGUZI, HAKI ZA BINADAMU NA MSAADA WA KISHERIA KUPITIA NANENANE

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025, Wizara ya Katiba na Sheria imetumia Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ya Nanenane kama jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu katiba, sheria za uchaguzi, haki za binadamu pamoja na huduma za msaada wa kisheria.


Akizungumza Agosti 1, 2025 kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Sheria kwa Umma kutoka wizara hiyo, Mhe. Abdulrahman Msham, amesema elimu hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kuelewa haki, wajibu na miongozo ya kisheria kabla na baada ya uchaguzi.


“Tunatoa elimu kuhusu katiba, sheria za uchaguzi, na haki za binadamu. Lakini pia kupitia kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, tunashughulikia migogoro mbalimbali ya wananchi, kutoa ushauri wa kisheria, na hata kusaidia wale wanaotaka kuomba kuongezewa muda kufungua mashauri mahakamani,” amesema Mhe. Msham.


Amesema wizara pia inasimamia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (Alternative Dispute Resolution – ADR) kwa kusajili na kutoa elimu kwa watu wanaotaka kuwa watatuzi wa migogoro, jambo linalosaidia kupunguza msongamano wa kesi mahakamani na kutatua migogoro kwa haraka.


“Mbali na migogoro, tunatoa elimu ya haki za binadamu, pamoja na ulinzi wa maliasili na utajiri wa asili wa nchi yetu. Haya ni mambo ya msingi kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa letu,” alifafanua.


Mhe. Msham alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi wote wanaotembelea maonesho ya Nanenane mwaka huu kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata huduma hizo muhimu bure.


“Huduma zote tunazozitoa hapa ni bure. Tunao wataalamu waliobobea katika masuala ya sheria ambao watakuhudumia papo kwa hapo. Changamoto zako za kisheria zitamalizika hapa hapa,” alisisitiza.


Maonesho ya mwaka huu yamebebwa na Kaulimbiu isemayo Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025,” ikilenga kuhamasisha wananchi kuchagua viongozi wenye maono ya kuinua sekta za uzalishaji – hasa kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu.


Wizara ya Katiba na Sheria imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanapata uelewa wa masuala ya kisheria kwa wakati sahihi, na ushiriki wao katika maonesho haya unaendelea kuimarisha uhusiano baina ya Serikali na wananchi katika kujenga taifa linalozingatia utawala wa sheria.


🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post