WAZIRI MKUU MAJALIWA APONGEZA JITIHADA ZA COOP BANK KATIKA KUIUNGA MKONO SEKTA YA KILIMO

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa leo ametembelea Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambapo amekagua mabanda mbalimbali ya taasisi, makampuni na wadau wa maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.


Akiwasili katika banda la Benki ya Ushirika Tanzania (Coop Bank), Waziri Mkuu alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Godfrey Ng’urah, ambaye alimweleza kwa kina namna benki hiyo inavyotekeleza kwa vitendo dhamira yake ya kuboresha huduma za kifedha kwa wakulima na wadau wote wa mnyororo wa thamani wa kilimo-biashara.


Katika mazungumzo yao, Bw. Ng’urah alibainisha kuwa Coop Bank imejipambanua kama benki inayojielekeza moja kwa moja katika kuhudumia sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo nafuu, ushauri wa kifedha, pamoja na kuwawezesha wakulima wadogo, vijana na wajasiriamali vijijini kuwa na mitaji endelevu ya kuendeleza shughuli zao.


"Benki yetu imejikita katika kutoa huduma bunifu zinazogusa moja kwa moja maisha ya Watanzania wa kawaida hasa wanaojishughulisha na kilimo, mifugo na uvuvi. Tunahakikisha wakulima wanapata fedha kwa wakati, kwa masharti nafuu na kwa njia rahisi kupitia mifumo ya kidijitali na ushirikiano na vyama vya msingi," alisema Bw. Ng’urah.


Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa aliipongeza Coop Bank kwa mchango wake mkubwa katika kuinua sekta ya kilimo nchini na kuonesha mfano wa taasisi za kifedha zinazochangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa kupitia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.


"Serikali inathamini sana mchango wa taasisi kama Coop Bank katika kufanikisha agenda ya uchumi wa viwanda kwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo. Natoa wito kwa taasisi nyingine za kifedha kuiga mfano huu," alisisitiza Waziri Mkuu.


Pamoja na kukagua mabanda ya maonesho, Waziri Mkuu pia amezungumza na wanachama wa ushirika na kuwapatia tuzo, zawadi na vyeti, leo Agosti 03, 2025.


Maonesho ya Nanenane mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi 2025"




🚨Subscribe YOUTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.


Previous Post Next Post