Na Carlos Claudio, Dodoma.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza kuwa tayari imetoa zaidi ya Shilingi trilioni 1.1 kwa ajili ya mikopo kwa wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha kilimo cha kibiashara kupitia huduma za kifedha jumuishi.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Biashara wa TADB Kanda ya Kati, Bi. Mariam Leonard, amesema benki hiyo inatumia maonesho hayo kama fursa ya kutoa elimu kwa wakulima kuhusu upatikanaji wa mikopo ya moja kwa moja pamoja na huduma nyingine za kifedha zinazolenga kukuza sekta ya kilimo.
“Benki tayari imetoa zaidi ya Shilingi trilioni 1.1 kwa wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo. Tunataka kuona kila mkulima anapata nafasi ya kukuza shughuli zake kupitia mikopo na elimu tunayoitoa,” alisema Bi. Mariam.
TADB imekuwa mstari wa mbele kuhimiza ushiriki wa wanawake na vijana katika kilimo cha kisasa na chenye tija, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuongeza uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao, na kuchochea uchumi wa kilimo nchini.
Aidha, benki hiyo imekuwa ikitekeleza kwa mafanikio mpango wa Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS), unaolenga kuwawezesha wakulima waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya dhamana kupata mikopo kupitia taasisi 19 za kifedha washirika.
Maonesho ya Nanenane mwaka huu yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wakulima na wadau wa maendeleo katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kupitia maonesho hayo, wakulima wanapata maarifa mapya kuhusu teknolojia za kisasa, fursa za masoko, na huduma za kifedha kama zile zinazotolewa na TADB.
Kauli mbiu ya mwaka huu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”imejikita katika kuhamasisha uwajibikaji, uongozi bora, na mchango wa sekta ya kilimo katika maendeleo ya taifa.
Bi. Mariam ametoa wito kwa wananchi wanaotembelea maonesho hayo kufika katika banda la TADB ili kujifunza zaidi kuhusu fursa zinazopatikana, akisisitiza kuwa benki hiyo ipo kwa ajili ya kumsaidia mkulima kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara chenye faida.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.