CMSA YAENDELEA KUCHOCHEA MAENDELEO KUPITIA MASOKO YA MITAJI – YAISHAURI JAMII KUKUZA UWEKEZAJI WA PAMOJA



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeendelea kuonesha jitihada thabiti katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha kutoka kwa wawekezaji binafsi na kuzielekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi shirikishi unaogusa wananchi moja kwa moja.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Meneja wa Mahusiano na Elimu kwa Umma wa CMSA, Bw. Charles Shirima, alisema kuwa masoko ya mitaji ni jukwaa muhimu kwa wananchi na wajasiriamali kupata mitaji ya maendeleo, huku akiisisitiza jamii kuchangamkia fursa hizo kwa kujiandaa vizuri kisheria na kitaasisi.


"Ili kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa pamoja, ni muhimu kwa wananchi kuwa na nyaraka rasmi ikiwemo Katiba ya kikundi pamoja na mpango kazi wa utekelezaji. Hili ni jambo la msingi katika kujenga misingi ya kisheria na uwazi wa uendeshaji wa uwekezaji wao," alisema Bw. Shirima.


Katika kuhakikisha elimu ya uwekezaji inawafikia wengi, CMSA imekuja na mbinu bunifu ya kuwahusisha vijana na wanafunzi wa elimu ya juu kwa kuandaa mashindano maalumu ya uwekezaji


Kupitia mashindano hayo, wanafunzi watajifunza misingi ya masoko ya mitaji, na washindi watapata nafasi ya kuwekeza fedha walizoshinda, hatua itakayowajengea uelewa na kuanza safari ya kuwa wawekezaji mahiri mapema.


"Mashindano haya yana lengo la kuibua kizazi kipya cha wawekezaji. Tunataka kuona vijana wakichukua nafasi katika uchumi wa nchi kupitia masoko ya mitaji," aliongeza.


CMSA imekuwa mdau muhimu katika kujenga mazingira wezeshi ya kiuchumi, huku ikitoa elimu ya mara kwa mara kwa jamii ili kuhakikisha kila Mtanzania anaelewa na anafaidika na uwekezaji wa pamoja, dhamana, hisa na bidhaa nyingine za kifedha zinazopatikana kupitia masoko rasmi ya mitaji.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post