TAKWIMU NI NGUZO YA MAENDELEO, NBS YAWAHIMIZA WATANZANIA KUZITUMIA

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Idara ya Mawasiliano na Usambazaji kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa wito kwa Watanzania na Asasi za Kiraia kutumia takwimu sahihi katika kupanga na kufuatilia miradi ya maendeleo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 iliyoizinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Akizungumza jijini Dodoma katika Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Afisa Mawasiliano wa NBS, Andrew Punjila, alisema takwimu ni chachu ya maendeleo kwa kuwa zinatoa msingi wa kupanga miradi kwa ushahidi.


“Tunatumia fursa hizi kuwaelimisha wananchi na wadau kuhusu umuhimu wa takwimu. Kupitia takwimu tunaweza kubaini changamoto na fursa zilizopo, kupanga mikakati madhubuti na kufuatilia maendeleo ya Taifa,” alisema Punjila.


Aliongeza kuwa takwimu za idadi ya watu kwa umri na jinsia, takwimu za mazingira, elimu, kilimo na huduma za jamii, zinatoa mwongozo wa kutekeleza miradi kwa ufanisi.


Punjila alisema sensa ya watu na makazi imekusanya taarifa muhimu zitakazosaidia katika kupanga matumizi bora ya rasilimali, kuimarisha kilimo cha kisasa chenye tija, kulinda mazingira, kuimarisha uhakika wa chakula, na kuendeleza viwanda vidogo kuanzia ngazi ya mitaa.



Alisema takwimu pia zinaweza kutumika na mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo kupata fedha za kufadhili miradi yao, kwa kuwa zinatoa ushahidi wa mahitaji halisi katika maeneo husika.


“Hata ninyi waandishi wa habari mnahimizwa kutumia takwimu katika maudhui yenu. Takwimu zinapoongezwa kwenye taarifa, zinaipa nguvu na kuifanya iwe na uhalisia unaosaidia watu kufanya maamuzi sahihi,” alisema.


Aidha, alihimiza wananchi kutembelea tovuti ya NBS (www.nbs.go.tz) na maktaba yao ili kupata machapisho na taarifa mbalimbali zilizotokana na tafiti na sensa, akibainisha kuwa serikali imewekeza kikamilifu katika ukusanyaji na usambazaji wa takwimu kwa maendeleo ya Taifa.


Kwa mujibu wa Punjila, matumizi ya takwimu sahihi yataisaidia Tanzania kufanikisha malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya 2050, ikiwemo kuboresha afya, huduma za jamii, upatikanaji wa umeme, kilimo endelevu, na uchumi shirikishi unaonufaisha wananchi wote.





🚨Sunscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post