BITEKO: WATANZANIA HAWANA SABABU YA KUOGOPA KUPIKA KWA UMEME

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema Watanzania hawana sababu ya kuogopa kutumia umeme kupikia, kwani nishati hiyo ipo ya kutosha, salama na sasa kuna vifaa vinavyotumia umeme kidogo kupika chakula kwa ufanisi.


Akizungumza leo Agosti 14, 2025 jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa programu ya utoaji majiko ya umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Biteko alisema kwa sasa Watanzania wanaotumia umeme kupikia ni asilimia 4.2 pekee.


“Ni ukweli kwamba, kwa historia na mazoea tuliyonayo, watu wanaamini kutumia umeme kupikia ni ghali. Tafiti zinaonesha majiko janja ya umeme yanaweza kutumia chini ya uniti moja sawa na shilingi 352 kuandaa mlo mmoja, tofauti na kutumia mkaa unaogharimu shilingi 2,000 hadi 3,000,” alisema.


Dkt. Biteko alifafanua kuwa matumizi ya umeme kupikia yanafanana na gharama za kuendesha balbu ya umeme nyumbani, hivyo ni nafuu na rafiki kwa mazingira.


Aliwataka wafanyakazi wa TANESCO kuwa wabunifu, kusimamia shirika kwa weledi na kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia. “Kila mfanyakazi anapaswa kuona fahari kutumia umeme badala ya kuni au mkaa, ili muwe mfano wa kuishi mnayoyahubiri,” alisema.


Awali, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Balozi Zuhura Bundala, alisema lengo la shirika ni kuchangia juhudi za kitaifa kuhakikisha kufikia mwaka 2034 Watanzania angalau asilimia 80 wanatumia nishati safi ya kupikia.


Naye Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema shirika limezindua majiko ya kisasa yanayotumia umeme mdogo na kupika haraka, ambapo majiko 100,000 yatatolewa kwa wafanyakazi kwa bei ya ruzuku ili wawe mabalozi wa teknolojia hiyo.


Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa TANESCO, menejimenti ya Wizara ya Nishati na wafanyakazi wa shirika hilo.




🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post