TADB YAVUNJA VIKWAZO VYA MIKOPO KWA WAKULIMA WADOGO – ZAIDI YA WAKULIMA 700,000 WANUFAIKA

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuonyesha dhamira yake ya dhati katika kuinua sekta ya kilimo nchini kupitia utoaji wa mikopo nafuu yenye masharti rafiki kwa wakulima wadogo, wafugaji na wavuvi, kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (SCGS).


Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Biashara wa TADB, Bi. Rosemary Gordon, amesema mfuko huo ulioanzishwa mwaka 2018 umewanufaisha wakulima 762,291 nchini kote kwa kuwawezesha kupata mikopo kupitia taasisi 19 za kifedha, zikiwemo benki na taasisi za kifedha ndogo.


“Changamoto ya ukosefu wa dhamana imekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima wetu nchini. Kupitia SCGS, tunashirikiana na taasisi za kifedha kutoa dhamana ili kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi,” alisema Bi. Rosemary.


Alifafanua kuwa TADB hutoa mikopo katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji mashambani hadi uchakataji na uuzaji wa mazao. 


Zaidi ya Shilingi bilioni 197 zimetumika kufadhili pembejeo kama mbegu, mbolea na viuatilifu, huku zaidi ya bilioni 43.6 zikitolewa kwa ajili ya ununuzi wa matrekta na vifaa vingine vya kisasa vya kilimo.


“Lengo letu ni kuhakikisha kila mhusika katika mnyororo wa kilimo anapata fursa ya kujikomboa kiuchumi. Tunatoa mkopo hata kwa wale wanaochakata mazao, wanaosafirisha na kuuza – wote hawa wanapata dhamana kupitia SCGS,” aliongeza.


Bi. Rosemary pia alieleza kuwa mfuko huo hauwahudumii wakulima pekee bali pia wafugaji wa kuku, ng’ombe wa maziwa, na wale wanaojihusisha na unenepeshaji wa mifugo, wakifaidika kupitia dhamana ya mkopo.


Kwa mujibu wa Bi. Rosemary, mfuko huu tayari umefanya kazi katika mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar, huku TADB ikitoa mwito kwa washiriki wa Maonesho ya Nanenane mwaka huu kufika katika banda la benki hiyo ili kupata elimu zaidi juu ya huduma hizo.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwajumuisha wanawake na vijana katika mapinduzi ya kilimo, akisema TADB inatoa dhamana ya hadi asilimia 70 kwa miradi ya vijana na wanawake inayozingatia kilimo rafiki kwa mazingira (climate-smart agriculture).


“Tunahamasisha vijana na wanawake kutumia fursa hii ya kipekee ya dhamana ya mkopo. Ni muda wa kuchukua hatua na kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa kilimo,” alihitimisha Bi. Rosemary.


🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post