SERIKALI YAZINDUA DIRISHA LA MIKOPO KWA VIJANA KILIMO – COOP BANK YAPOKEA BIL. 8.5 KUWEZESHA KILIMO CHA KISASA


Na Carlos Claudio, Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao, Usalama wa Chakula na Ushirika, Dkt. Stephen Nindi, ameihimiza Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank) kuhakikisha inasimamia kwa makini urejeshaji wa mikopo kwa vijana wanaojiingiza katika kilimo ili fedha hizo ziweze kuwanufaisha vijana wengine nchini.


Dkt. Nindi alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Dirisha Maalum la Mikopo kwa Vijana, lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano katika Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) Nzuguni, mkoani Dodoma.


Tunaitaka Benki ya Ushirika Tanzania kuweka mfumo bora wa usimamizi wa mikopo, hasa kwa vijana. Wanaokopa lazima warejeshe, ili fedha hizi ziwasaidie wengine. Huu ndio msingi wa maendeleo ya kweli katika sekta ya kilimo,” alisema Dkt. Nindi.


Katika hafla hiyo, Benki ya Ushirika Tanzania ilipokea hundi ya Shilingi Bilioni 8.5 kutoka Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu kwa vijana, wanawake na vyama vya ushirika vinavyojihusisha na shughuli za kilimo na biashara.


Fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano baina ya Wizara ya Kilimo na COOP Bank, yaliyolenga kuongeza mitaji rafiki kwa wakulima na kukuza kilimo cha kisasa kinachozingatia tija na ushindani.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa COOP Bank, Bw. Godfrey Ng’ura, alisema kuwa dirisha hilo limebuniwa mahsusi kwa ajili ya kuwafikia vijana, wanawake, Vyama Vikuu vya Ushirika (AMCOS), Vyama vya Msingi na Vyama vya Kifedha vya Kijamii, ili waweze kupata mikopo yenye masharti nafuu.


Tumezindua pia huduma ya kipekee iitwayo ‘Mchongo Shambani’ kwa ajili ya vijana na wanawake walioshiriki katika mpango wa BBT (Build a Better Tomorrow), ambapo mikopo hiyo itatolewa kwa riba ya chini isiyozidi asilimia 9,” alisema Bw. Ng’ura.


Huduma hii inalenga kuongeza fursa kwa vijana wengi kushiriki katika shughuli za kilimo biashara kwa kutumia teknolojia, mitaji na mbinu za kisasa zinazowezesha tija kubwa katika uzalishaji.


Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa vijana na makundi maalum yanapata nafasi katika sekta ya kilimo, huku ikihimiza taasisi za fedha kuandaa bidhaa na huduma zitakazowawezesha kushiriki ipasavyo katika mnyororo wa thamani wa kilimo.


Uzinduzi wa dirisha hilo ni sehemu ya juhudi za pamoja baina ya serikali na sekta ya fedha kuhakikisha kilimo kinakuwa chenye tija, ajira na maendeleo kwa Watanzania wote.






🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post