WIZARA YA KILIMO YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TUME YA HAKI ZA BINADAMU KUTATUA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Wizara ya Kilimo imeeleza dhamira yake ya kushirikiana kwa karibu na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) katika kulinda haki za binadamu, hususan haki ya kuishi katika maeneo yenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Athuman Kilundunya, wakati alipotembelea banda la THBUB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.


Wizara ya Kilimo ipo tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, hasa kwenye maeneo yenye migogoro kati ya wakulima na wafugaji. Katika baadhi ya maeneo, migogoro hiyo imekuwa ikiathiri haki ya msingi ya kuishi, alisema Mhandisi Kilundunya.



Mhandisi Kilundunya alibainisha kuwa Wizara imekuwa mstari wa mbele kupambana na migogoro hiyo, lakini ni muhimu kushirikiana na taasisi kama THBUB ili kupata ushauri na mapendekezo yatokanayo na uchunguzi wa kina wa matukio yanayokiuka haki za wakulima na wafugaji.


Tushirikiane katika kutatua migogoro hii. THBUB mnaweza kutuletea ushauri kutokana na chunguzi mnazozifanya, ili kwa pamoja tusaidie wananchi wetu,” aliongeza.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu kwa Umma na Mawasiliano wa THBUB, Bi. Zawadi Msalla, alisema kuwa Wizara ya Kilimo ni mdau muhimu wa Tume hiyo na wamekuwa wakishirikiana katika masuala mengi yanayohusu usimamizi wa haki za binadamu katika sekta ya kilimo.


Tumejenga uhusiano mzuri na Wizara ya Kilimo na tunajivunia ushirikiano huu. Tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi ili kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa, hususan katika maeneo ya vijijini ambako migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji ni ya mara kwa mara,” alisema Bi. Zawadi.


Aidha, alieleza kuwa THBUB imeshiriki katika Maonesho ya Nanenane mwaka huu kwa lengo la kutoa elimu ya haki za binadamu, kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi na kupokea malalamiko mbalimbali yahusuyo uvunjwaji wa haki na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.


Kwa pamoja, Wizara ya Kilimo na THBUB wameahidi kuimarisha mashirikiano ili kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na migogoro kati ya wakulima na wafugaji inapatiwa suluhisho la kudumu.


🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post