Na Carlos Claudio, Dodoma.
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imefanikiwa kupunguza gharama za huduma za uchujaji damu kwa wagonjwa wa figo kutoka zaidi ya shilingi laki tatu kwa mara moja miaka mitatu iliyopita, hadi shilingi laki mbili sasa, huku ikilenga kushusha gharama hizo hadi chini ya laki moja.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mhe. Gerson Msigwa, amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kuimarisha huduma za afya na kupunguza mzigo wa gharama kwa wananchi.
“Serikali inaendelea kuongeza mashine za uchujaji damu na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma kwa gharama nafuu. Malengo yetu ni kushusha gharama zaidi na kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema Msigwa.
Kwa upande wa upatikanaji wa dawa, MSD imeimarisha huduma zake kwa kuongeza vituo vya usambazaji kutoka 7,195 mwaka 2021 hadi kufikia 8,876 mwaka huu, sawa na ongezeko la vituo 1,681 ndani ya miaka minne pekee.
Msigwa amesema zamani baadhi ya vituo vya afya na zahanati vilikuwa havipati dawa kwa wakati, hali iliyosababisha baadhi ya dawa kuharibika kabla ya kutumika, lakini sasa changamoto hiyo imepatiwa ufumbuzi.
“Kwa sasa, kituo chochote cha afya kinachoagiza dawa MSD, tunahakikisha zinapatikana kwa wakati. Dawa siyo bidhaa za majaribio, ni lazima ziwe salama na zifike kwa wakati ili kuokoa maisha,” alisisitiza.
Serikali pia imekamilisha ujenzi wa maghala mapya ya dawa katika mikoa ya Dodoma na Mtwara, kwa gharama ya shilingi bilioni 42, hatua itakayoongeza uwezo wa kuhifadhi na kusambaza dawa kwa ufanisi zaidi.
Kwa mujibu wa Msigwa, MSD inaendelea pia kuimarisha uwezo wa kuzalisha dawa ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.