Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoanza Agosti 28 mwaka huu zinafanyika kwa amani na kuepuka matumizi ya lugha za matusi au vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Akizungumza leo (Agosti 18) jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua mafunzo kuhusu sheria na gharama za uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa, Jaji Mutungi amesema vyama vina wajibu wa kuendeleza mshikamano wa taifa.
“Amani na umoja wa kitaifa viwe kipaumbele kwenu. Twendeni tukawe mabalozi wa amani,” amesema Jaji Mutungi.
Aidha, amewataka viongozi wa vyama kuongeza uelewa kwa wagombea wao ili washiriki vyema katika mchakato wa uchaguzi, huku akisisitiza umuhimu wa kampeni za kistaarabu bila matusi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CPA Edmund Mgasha, amewataka viongozi wa vyama kuzingatia uwazi wa matumizi ya fedha kwa kuweka ushahidi na akaunti maalum za uchaguzi. Ameonya pia dhidi ya vitendo vya rushwa na kutoa au kupokea zawadi ili kushawishi wapiga kura.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ameomba Ofisi ya Msajili kutafsiri sheria za uchaguzi kwa Kiswahili ili kuongeza uelewa kwa wadau. Hata hivyo, amesema utekelezaji wa sheria za gharama za uchaguzi ni changamoto kutokana na ofisi hiyo kutozifikia mikoa mingi.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.