MFUKO WA PEMBEJEO WAKABIDHI BILIONI 8.5 KWA BENKI YA USHIRIKA KWA AJILI YA MIKOPO KWA WAKULIMA



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Katika hatua ya kuendeleza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuinua sekta ya kilimo nchini, Mfuko wa Pembejeo umekabidhi kiasi cha shilingi bilioni 8.5 kwa Benki ya Ushirika Tanzania (COOP Bank)kwa ajili ya kuwezesha wakulima kupata mikopo nafuu ya pembejeo na mitaji ya kilimo.


Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Itandula Gambalagi, alisema fedha hizo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati ya Mfuko na COOP Bank kupitia Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa Aprili 2025 mbele ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima, leo tunakabidhi mfano wa hundi ya shilingi bilioni 8.5 kwa Benki ya Ushirika. Kati ya fedha hizo, bilioni 5 ni mkopo wa jumla wa miaka mitano wenye riba nafuu ya asilimia 3,” alisema Bw. Gambalagi.


Kwa mujibu wa Gambalagi, sehemu ya fedha hizo itatumika kama dhamana ya mikopo (Credit Guarantee) ili kusaidia wakulima wadogo ambao hawana dhamana au dhamana zao hazitoshelezi kupata mikopo kutoka Benki ya Ushirika. Aidha, akaunti maalum ya uendeshaji tayari imefunguliwa katika benki hiyo ili kurahisisha utekelezaji wa makubaliano hayo.


Benki ya Ushirika itakuwa na jukumu la kupokea, kuchakata na kuidhinisha maombi ya mikopo kwa niaba ya Mfuko wa Pembejeo, pamoja na kutoa taarifa za kila mwezi kuhusu:

  • Majina ya wanufaika,
  • Kiasi cha mkopo,
  • Mahali walipo (mkoa na wilaya),
  • Madhumuni ya mkopo,
  • Muda wa mkopo na taarifa za marejesho.

Mashirikiano haya yanalenga kuongeza kasi ya utoaji mikopo kwa wakulima wengi zaidi kupitia COOP Bank, yenye matawi manne na mawakala walioko karibu na wakulima,” alifafanua Bw. Gambalagi.


Bw. Gambalagi alitumia nafasi hiyo kuitaka COOP Bank kuhakikisha usimamizi madhubuti wa fedha hizo, ili ziweze kuleta matokeo chanya kwa wakulima na kwa uchumi wa taifa kwa ujumla.


Fedha hizi za umma zinapaswa kutumika kwa ufanisi ili kuongeza uzalishaji, kuongeza ajira, na kuinua kipato cha kaya. Tunatarajia kuona wakulima wengi zaidi wakinufaika moja kwa moja na mikopo hii yenye masharti nafuu, alisisitiza.


Kwa mara nyingine, aliishukuru Benki ya Ushirika kwa ushirikiano mzuri na akatoa rai kwa wadau wote kuhakikisha kuwa mkakati huu unatekelezwa kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia vipaumbele vya wakulima wadogo.


Hatua hii ya Mfuko wa Pembejeo kushirikiana na Benki ya Ushirika ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kutumia mbinu za kifedha zenye tija kwa mkulima wa kawaida. Kwa mikopo hii ya riba nafuu, wakulima sasa wanapata nguvu ya kubadilisha maisha yao kupitia kilimo chenye tija na kisasa.



🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post