Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amelitaka Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi, hususan vijijini, ili kuongeza uelewa juu ya huduma hizo muhimu.
RC Senyamule alitoa wito huo Agosti 5, 2025, alipotembelea banda la EWURA CCC katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Afisa Uelimishaji na Uhamasishaji wa baraza hilo, Ligiko Lugiko, alisema EWURA CCC ina mkakati wa miaka 10 (2024–2034) unaolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
"Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kitu halisi na kinawezekana. Watu sasa wanaweza kupika kwa umeme au gesi, na huduma hizi zinapatikana kwa bei nafuu kwa Watanzania walio wengi," alisema Lugiko.
Aliongeza kuwa matumizi ya nishati safi yana faida kubwa kiafya, ikiwemo kupunguza magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda hilo walipongeza EWURA CCC kwa elimu waliyopewa, wakisema imewafungua kifikra kuhusu namna ya kushughulikia malalamiko yanayohusu huduma za umeme, maji, gesi na petroli.
"Hatukujua kama kuna chombo kinachoweza kututetea kwenye huduma tunazopata. Wakati mwingine tunapata changamoto, lakini hatuna pa kupeleka malalamiko yetu," alisema mmoja wa wananchi.
EWURA CCC ilianzishwa chini ya Kifungu Na. 30 cha Sheria ya EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania, kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi ya watumiaji wa huduma za nishati na maji nchini.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA