*◼️Mifugo yenye thamani ya takribani Mil. 50.5 yashindanishwa*
*◼️Yupo Mbuzi anayezalisha lita 24 za maziwa kwa siku*
Na Jasmine Shamwepu Dodoma.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendesha paredi maalum ya Mifugo kwenye Maonesho ya kimataifa ya Nane Nane 2025 kwa lengo la kuwahamasisha wafugaji kuachana na ufugaji wa asili na kugeukia ufugaji wa kibiashara.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia paredi hiyo Mgeni rasmi wa tukio hilo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Wizara hiyo kwa kufanya tukio hilo kuwa na hadhi ya kimataifa ambapo jumla ya Mifugo 27 ilishindanishwa.
“Paredi hii imekuwa chachu ya kubadili maisha ya wafugaji kwa kuwahamasisha kutumia teknolojia na mbinu za kisasa na kuzingatia uzalishaji wenye tija” Ameongeza Mhe. Senyamule.
Aidha Mhe. Senyamule amewataka wafugaji hao kuchangamkia fursa ya masoko ya mazao ya Mifugo ndani na nje ya nchi huku wakiendelea kuboresha mifugo yao kulingana na mahitaji ya masoko hayo ikiwa ni pamoja na kuchanja na kutambua mifugo yao.
“Lakini pia nimeona wafugaji wameanza kubadilika kwenye suala la malisho ya mifugo yao na sasa niwaelekeze Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili mabwawa yaliyopo kwenye maeneo yenu badala ya kukaa bila matumizi yoyote yaelekezwe kwenye shughuli za Mifugo na Uvuvi” Amesema Mhe. Senyamule.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amesema kuwa mabadiliko makubwa ya Paredi ya mwaka huu ni ishara ya kukua kwa sekta ya Mifugo na Uvuvi ambapo amewataka wafugaji kutumia mafunzo waliyopata kwenye tukio hilo kama darasa la kubadili mfumo wao wa ufugaji kwenye maeneo yao.
“Sekta zetu zimeendelea kuwekeza kwenye teknolojia kama tulivyoona hivyo wito wa wizara ni kuwasihi wadau mbalimbali wa sekta hizi kuchangamkia fursa za teknolojia hizi ili mwakani mje na matokeo yanayotokana na teknolojia hizi” Ameongeza Dkt. Mhede.
Aidha Dkt. Mhede amesema kuwa Paredi hiyo mbali na kuhamasisha ufugaji wa kibiashara inalenga kuinua hali ya lishe kwa wananchi kupitia ulaji wa mazao ya Mifugo na Uvuvi ikiwa ni pamoja na nyama, samaki, maziwa na mayai.
Paredi iliyofanyika mwaka huu ni ya 15 tangu kuasisiwa kwake na Rais wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete kwenye kilele cha Maonesho ya Nane Nane mwaka 2010.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.