Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) imefanikiwa kudhibiti kwa kiwango kikubwa uvuvi haramu katika Bahari Kuu ya Tanzania, hatua iliyowezesha ongezeko la mapato ya taifa mara kumi pamoja na kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta ya uvuvi.
Akizungumza katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa DSFA, Dkt. Emmanuel Sweke, alisema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya teknolojia ya kisasa ya ufuatiliaji wa meli (TEGA), ambayo inatoa taarifa kwa wakati halisi kuhusu shughuli za uvuvi katika eneo la bahari kuu lenye zaidi ya kilomita 2,000.
“Kwa sasa hakuna uvuvi haramu katika bahari kuu ya Tanzania. Mifumo yetu ya ufuatiliaji imerahisisha usimamizi wa meli zote zilizosajiliwa na kupata leseni kutoka Tanzania. Meli yoyote inapotia nanga katika maji yetu, inapaswa kutoa taarifa ndani ya saa 24,” alieleza Dkt. Sweke.
Alisema, DSFA ndiyo taasisi pekee yenye mamlaka ya kusimamia uvuvi katika bahari kuu, ikiwa na makao makuu yake Zanzibar, na kwamba taasisi hiyo hutoa pia ushauri wa kisera kwa Serikali kuhusu masuala yanayohusu sekta ya uvuvi katika maji ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Dkt. Sweke, DSFA inasimamia meli zote zinazotumia bendera ya Tanzania zinazovua samaki wanaohama kwa kasi (highly migratory species) kama vile jodari, na kwamba taasisi hiyo hushirikiana kwa karibu na nchi nyingine kuhakikisha uhifadhi endelevu wa rasilimali hizo.
Katika kufafanua hatua zilizochukuliwa dhidi ya ukiukwaji wa sheria, Dkt. Sweke alisema tangu mwaka 2018, DSFA iliwahi kukamata meli moja iliyopatikana na samaki aina ya papa — ambao ni miongoni mwa spishi zilizo hatarini kutoweka.
“Kwa mujibu wa sheria, samaki hawa hawaruhusiwi kuuawa. Iwapo atakufa, unatakiwa kumrejesha baharini na kutoa taarifa mara moja. Hii inaonesha ni kwa namna gani usimamizi wetu umeimarika,” alisisitiza.
Kwa sasa, ongezeko la maombi ya leseni za uvuvi wa bahari kuu linaashiria kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi katika mfumo wa usimamizi wa DSFA.
Dkt. Sweke alisema mafanikio hayo si tu yanawanufaisha wavuvi, bali pia yanaongeza mapato ya taifa na kulinda kwa ufanisi rasilimali za bahari kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu ya WASHINDI MEDIA