SENYAMULE: BOMBA LA MAFUTA NI NEEMA KWA KONDOA

 


Na Carlos Claudio, Kondoa Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema mradi wa kimkakati wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga kupitia wilaya ya Kondoa ni fursa ya kipekee kwa wananchi wa mkoa huo, hususan katika maeneo ya ajira, biashara na maendeleo ya miundombinu.


Akizungumza wakati wa ziara yake wilayani Kondoa, Mhe. Senyamule ametembelea mradi huo mkubwa wa kitaifa na baadaye kuzindua nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari ya Bolisa, ambapo alisisitiza dhamira ya Serikali kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi wa Dodoma.


“Tulianza ziara yetu asubuhi kwa kutembelea mradi wa bomba la mafuta ambao ni kati ya miradi mikubwa ya kimkakati nchini. Mkoa wa Dodoma una bahati kubwa kwa kuwa bomba hili linapita katika wilaya ya Kondoa na Chemba, jambo linalowapa wananchi wetu fursa ya kiuchumi na kijamii,” amesema Mhe. Senyamule.



Mradi wa bomba la mafuta (East African Crude Oil Pipeline - EACOP) utasafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi. Katika hatua hiyo, Tanzania na Uganda zitashirikiana kuhakikisha utekelezaji wa mradi unazingatia maslahi ya wananchi.


Kwa mujibu wa Mhe. Senyamule, tayari wafanyakazi zaidi ya 350 wamejengwa katika kambi maalum wilayani Kondoa wakihusika moja kwa moja na ujenzi wa bomba hilo, hatua inayochangia ongezeko la ajira na biashara kwa wananchi wa eneo hilo.


“Mradi huu unawaletea wananchi wa Kondoa fursa nyingi kama ajira, biashara, na ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na wataalamu wanaotekeleza ujenzi huu. Tunawahimiza wananchi kuutumia mradi huu kikamilifu kwa manufaa yao,” aliongeza.



Katika hatua nyingine ya ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa alizindua rasmi nyumba ya walimu katika shule ya sekondari ya Bolisa kama sehemu ya maboresho ya mazingira ya kufundishia na kujifunzia.


Amesisitiza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa maendeleo ya muda mrefu, na kwamba serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule hususan vijijini ili kuwavutia walimu na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.










🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post